Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Sept 8,2024
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya CCM, Ally Hapi (MNEC), ametuma salamu kwa viongozi waliochaguliwa ambao wameshindwa kuwajibika kwa maslahi ya wananchi na kusisitiza Chama cha Mapinduzi hakitambeba ambae habebeki wakati wa chaguzi Novemba 2024/2025.
Ameeleza ni wakati wa kwenda na wagombea wanaobebeka,wanaoweza kujiuza na sio mzigo kwa Chama kukipa kazi ya kuwasemea.
Akiendelea na ziara yake ya siku nne Mkoani Pwani, Hapi alieleza wanachama wajitokeze wanaokubalika, ambao wataivusha CCM na sio kukubalika kwenye mifuko ya watu.
“Chama chetu kina utaratibu mzuri katika chaguzi muda unapofika na kila muda wa uchaguzi ndiyo maana tunasisitiza suala la kupata wagombea wenye uwezo na bora tutakao wauza kwa urahisi ambae anakubalika na wananchi na siyo anayekubalika kwenye mifuko ya watu wachache, kiongozi ambaye anazijua shida za wananchi na uchaguzi wa serikali za mitaa ndiyo msingi wa uchaguzi mkuu” alisema Hapi .
Kuhusu viongozi wasiowajibika kwenye nafasi zao Hapi alieleza, katika kipindi kilichosalia kuelekea uchaguzi Mkuu ni muhimu kwa kila kiongozi aliyechaguliwa na wananchi kujitathimini iwapo anafaa kurejea katika nafasi yake kwenye uchaguzi ujao.
“Waheshimiwa madiwani , wabunge naomba mchape kazi muda ndiyo huu chama hakitambeba mtu ambaye hakujibeba yeye mwenyewe kwa utendaji kazi wake, ninachoomba mtambue ni kuwa unafika kwenye uchaguzi huchaguliwi wewe kwa sababu ni bingwa wa fitna au wewe ni bingwa wa kumsema vibaya mwenzio au wewe ni bingwa wa kujisemea wewe mwenyewe ,bali matendo yako na namna ulivyoshughulika na matatizo ya wananchi “
Hapi aliwaonya watu wanaojihusisha na udalali kwenye uchaguzi kwa kujifanya wao ndiyo kila kitu juu ya ushindi wa wagombea .
“Wapambe nuksi ndio wakati wao wasiwavuruge na wasivuruge Chama , hali hiyo imekuwa mzigo mkubwa kwa viongozi walioko madarakani na kusababisha washindwe kufanya kazi kwa ufasaha”
“Lakini wapo watu hapa ni madalali wa uchaguzi ambao wametengeneza upepo kwa mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi hiyo lazima amuone yeye na akiamini ushindi wa mgombea upo kwenye mikono yake, katika kipindi hiki jiepusheni na madalali wa siasa katika uchaguzi” anasisitiza Hapi.
Katika ziara hiyo Hapi,ameshapita wilaya ya Kibaha, Bagamoyo, septemba 8,2024 amefanya ziara hiyo ya kikazi Mkuranga na atakamilisha Rufiji septemba 9 mwaka huu.