NA FAUZIA MUSSA
WAKALA wa Chakula na Dawa (ZFDA), kwa kushirikiana na na wakaguzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar (AAKIA), wamekamata begi nne zenye dawa za binaadamu zilizoingizwa Nchini, zikitokea India kwa kutumia shirika la ndege la ethopia bila kufuata utaratibu.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na mzigo huo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Dawa na Vipodozi Sabrina Idrissa Ahmada alisema dawa hizo si salama kwa watumiaji kwani hazijasajiliwa na Taasisi husika (ZFDA).
Vilevile alieleza kuwa dawa hizo zilifungashwa katika kifungashio kisicho rasmi kusafirishia dawa na muingizaji wa dawa hizo si halali kutokana na kutosajiliwa na kufuata taratibu zilizowekwa.
Sabrina alizitaja baadhi ya dawa hizo kuwa ni pamoja na dawa za kutibu saratani, tenzi koo (goita), magonjwa ya akili na antibiotics.
kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ZFDA ilieleza kuwa baada ya kuingia nchini mzigo huo ulishughulikiwa na mtoa mizigo (agent) Nassor Humoud Nassor, ambae alidai kutokua na maelezo ya kutosha ya mmiliki halali wa mzigo huo baada ya kuhojiwa na wakaguzi hao.
Mbali na hayo Sabrina aliwaomba wadau mbalimbali ikiwemo wa sekta ya afya na vyombo vya habari kushirikiana katika kuhakikisha elimu na miongozo juu ya usalama wa dawa inafika katika ngazi zote za jamii kwa lengo la kulinda afya za watumiaji.
Kufuatia tukio hilo lililotokea Septemba 5, 2024, ZFDA imeziweka dawa hizo chini ya uangalizi na usimamizi maalum na kumtaka mtoaji wa wa mzigo huo (agent) kuwasilisha barua ya kujieleza pamoja na vielelezo vya uingizaji wa dawa hizo, ili taratibu nyengine za kisheria ziendelee kuchukuliwa.