Pia, amewatahadharisha wale wote wanaotaka kumpinga Rais Dk. Samia katika uchaguzi mkuu ujao, kuwa wajipange vizuri kutokana na kazi kubwa aliyofanya ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo daraja hilo refu na la kisasa.
Cheyo alitoa pongezi hizo leo alipowaongoza wanachama wa UDP kutembelea mradi wa daraja la J.P. Magufuli maarufu Kigongo-Busisi, linalojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 716.33.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mradi huo, Cheyo amesema kwamba UDP na wanachama wake wameridhishwa na furaha kwa kuona maono ya Hayati John Magufuli yakitekelezwa na Rais Dk. Samia kwa vitendo.
“Tunapotaka kusema jambo la kuisaidia serikali ifanye vizuri, si kupinga tu. Tuliona twende kwenye mradi mmoja kuona kodi zetu zinafanya nini. Daraja hili limejengwa kwa fedha za Watanzania na wanajivunia fedha zao kutumika kwa kazi kubwa na yenye manufaa,” amesema Cheyo.
Mwenyekiti huyo wa UDP, almaarufu Mzee Mapesa, amesema baada ya kutembelea mradi huo atawaambia Watanzania kuwa kodi yao imetumika vizuri katika ujenzi wa daraja hilo la kimkakati litakalotuunganisha kiuchumi na nchi zingine.
“Naipongeza serikali ya awamu ya sita kwa maono ya kutekeleza mradi huu. Watakaochukia shauri yao. Mwakani kuna uchaguzi mkuu; niwaambie wanaotaka kupishana na Dk. Samia kwa utekelezaji huu wa miradi ya kimkakati, wajiandae vizuri kwa kazi kubwa. Rais Samia ameteka mioyo ya watu,” ameongeza.
Pia, katika mradi huo, wahandisi wazawa wameonesha umahiri na uwezo, hivyo baada ya daraja hilo kukamilika, tunaweza kuamua kujenga miradi mingine ya aina hiyo kwa kutumia wataalamu wetu wenyewe bila kutegemea wahandisi wageni.
Mwenyekiti wa UDP Mkoa wa Kagera, Majaliwa Yusufu,amesema serikali imefanya kazi nzuri ya kujenga daraja hilo ambalo litaondoa changamoto ya kusubiri vivuko na kurahisisha usafiri na biashara. Hivyo, anamshukuru Rais Samia kwa kutekeleza maono ya mtangulizi wake.
Katibu Mwenezi wa UDP Mkoa wa Mwanza, Paulo Magilinga, amesema: “Tulikuwa tukisumbuka tukikosa kivuko. Kwa daraja hili, serikali iongeze kasi ya kulipa fedha za mkandarasi ili likamilike kwa wakati. Magufuli alionesha uzalendo na Mama Rais Dk. Samia ameendeleza maono hayo. Kikubwa, mkandarasi alipwe na akamlishe daraja kwa wakati. Katika uchaguzi wa mwakani, wakati wa kampeni tutapita hapa.”
Aidha, Katibu Mwenezi wa UDP Taifa, Erasto Nyaga, amesema: “UDP tumekuwa chama cha kwanza cha siasa kutembelea mradi wa Daraja la J.P. Magufuli na tutaendelea kutembelea mingine. Mama amefanya kazi nzuri; tumeona kodi zetu zilivyotumika ili tuwaeleze Watanzania. Tatizo ni kwamba wanaomzunguka wanakwenda kinyume, lakini ametekeleza maono vizuri. Anaendelea kutoa fedha za maendeleo, na hivyo wanaotaka kumpinga wana kazi.”
Awali, msimamizi wa mradi huo kutoka TANROADS, Mhandisi Devotha Kafuku, amesema mradi umefikia asilimia 90.5. Kupitia programu ya kuewaendeleza Watanzania, wapo asilimia 93, na mradi unatarajiwa kukamilika Desemba 2024.
“Daraja hili la kimkakati linaunganisha nchi ya Kenya kuanzia Sirari kupitia Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, na Kigoma, pia nchi za Burundi, Rwanda, DRC, na Uganda. Litakuwa na njia mbili za kwenda na kurudi pamoja na njia ya waenda kwa miguu,” amesema Mhandisi Kafuku.
Mhandisi Kafuku ameongeza kuwa daraja kuu kiunganishi linajengwa kwa teknolojia ya kisasa na serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa wataalamu waliojifunza kujenga madaraja bila kutegemea wageni, ingawa tatizo linaweza kuwa vifaa.
Aidha, Mhandisi Aloyce Kadokado amesema ujenzi wa Daraja la J.P. Magufuli umetekelezwa kwa viwango vya juu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya madaraja, lina nguzo tatu kuu ambapo zimebaki mita nane ili kuunganisha nguzo hizo kabla ya kumwaga lami.
“Upekee wa daraja hili ni kwamba ni refu na la sita Afrika, lina cable 12 za mwonekano wa kupendeza kwa bendera ya Tanzania, lina urefu wa km 3.2 na litafungwa taa za kumulika vizuri,” amesema Mhandisi Kadokado.