Kaimu Meneja wa MSD Kanda ya Magharibi Rashid Omari alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mkoani TABORA Ofisini kwake katika kuadhimisha miaka 30 Bohari ya dawa nchini .
Ni moja ya maghala ya kuhifadhi dawa katika bohari ya dawa kanda ya magharibi pichani ni msimamizi wa maghala MSD Tabora Veronica Okello .
Na Lucas Raphael,Tabora.
SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Magharibi imewahakikishia wakazi wa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi kuwa itaendelea kupeleka dawa za kutosha katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali za Wilaya hata kama halmashauri hazina pesa za kulipia kwa wakati huo.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Meneja wa MSD Kanda ya Magharibi Rashid Omari alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mkoani hapa katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Bohari ya Dawa nchini 1994.
Alisema kuwa huu ni mkakati wa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa zaidi ya asilimia 90 katika Kanda hiyo na maeneo mengine.
Aliongeza kuwa kupitia mkakati huu Bohari ya Dawa imejipanga kuhakikisha huduma za matibabu zinatolewa kikamilifu kwa jamii katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali zote zilizo chini ya Halmashauri za wilaya.
Omari alifafanua kuwa serikali ya awamu ya 6 inajali sana wananchi ndiyo maana MSD imekuja na mpango mkakati wa kuhudumia wananchi kwanza maslahi ya fedha yatafuata baadae.
Alibainisha kuwa Rais Dkt Samia alifanya maboresho makubwa sana katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya ya kutosha, zahanati na hospitali za wilaya tofauti na kipindi cha nyuma ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Meneja huyo ambaye Kitaaluma ni Mfamasia aliongeza kuwa kwa sasa MSD inasambaza dawa kila baada miezi 2 tofauti na zamani ambapo walikuwa wanasambaza dawa kila baada ya miezi 6.
Alieleza kuwa kwa kipindi cha mwaka 1 sasa wanasambaza dawa mara 6 nia na madhumuni ikiwa ni kuimarisha upatikanaji dawa katika vituo vya afya vyote na kuboresha miundombinu ya ufikishaji dawa hizo katika Vituo vyote mahali popote
‘Kwa sasaa kila baada ya miezi 2 MSD inasambaza tani 40 hadi 50 za dawa wakati huko nyuma tulikuwa tunasambaza tani 5 hadi 10 kila baada ya miezi 6, haya ni mabadiliko makubwa sana’, alisema.
Awali Meneja Mawasiliano na Uhusiano MSD Etty Kusiluka alieleza kuwa serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kusambaza dawa katika maeneo yote yenye Vituo vyote 8200 vya Kutolea huduma za afya nchini.
Alisema wamejipanga vizuri ili kuhakikisha inatoa zoezi la usamazaji dawa linafanyika kwa weledi mkubwa ili ziwafikie wananchi katika Kanda zote 10 zilizopo hapa nchini ikiwa Kanda ya Magharibi.
Aliongeza kuwa MSD imejenga maghahala makubwa ya kuhifadhia dawa katika Mikoa ya Dodoma na Mtwara ili kurahisisha usambazaji dawa katika Mikoa yote nchini na kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.