Mkaguzi wa Polisi Sada Salum ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe akiwa na Sajini wa Polisi Melina na Koplo wa Polisi Glady kwa pamoja wanetoa elimu ya madhara ya ukatili na matumizi mabaya ya mitandao kwa wanafunzi wa Kidato cha 05 shule ya Sekondari Vwawa Day.
Elimu hiyo imetolewa Agosti 28, 2024 kwa wanafunzi hao juu ya kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ikiwa ni ufunguzi wa kampeni maalum ya “TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIKA” ambayo inaendelea nchi nzima.
Vilevile wanafunzi hao wameelimishwa mambo mbalimbali yakiwemo madhara ya matumizi mabaya ya mitandao ikiwa ni pamoja na kuachana na kujihusisha na masuala ya mahusiano ya kimapenzi wangali wanafunzi na badala yake kuacha utoro na kusoma kwa bidii ili watimize ndoto za masomo na maisha yao ya baadae.
“Tumieni mitandao ili iwaletee tija katika masomo yenu na sio kuangalia na kufuatilia vitu ambavyo havina tija ikiwemo kuacha kurushiana video na picha za utupu ambazo ni kosa kisheria” alisema Mkaguzi Sada.
Aidha, wanafunzi hao wametakiwa kuendelea kuwa wazalendo na kutofanya uchochozi wa masuala mbalimbali kama vile Siasa na Dini pindi wawapo na watokapo shuleni kwani ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za Nchi.