Mkuu wa chuo cha Ualimu Patandi ,Lucian Segesela akizungumza na waandishi wa habari kwenye kongamano hilo.
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Watafiti wametakiwa kufanya tafiti katika eneo la watoto wenye ulemavu kwani changamoto nyingi zinazolikabili kundi hilo zinahitaji nguvu ya pamoja ili kufikia haki zao kuanzia kupata elimu hadi kupokea masomo nyumbani.
Mhadhiri na Mtaalamu wa masuala ya Jamii kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania Dkt. Mariana Makuu,amesema bado kuna mapungufu makubwa katika jamii kwani zimeendelea kuwanyanyapaa Watoto wenye ulemavu jambo ambalo amesema linachangia Watoto kutopelekwa shule.
Ameyasema hayo katika Kongamano la kitaaluma kuhusu Watoto wenye ulemavu na changamoto zao lililofanyika jijini Arusha,na kuwakutanisha wadau mbalimbali wawanaojihusisha na Watoto wenye ulemavu na kuainisha matokeo ya tafiti zilizofanyika jinsi ya kukabiliana na changamoto za Elimu Jumuishi na haki za Watoto wenye ulemavu.
Amesema kuwa, pamoja na elimu kuendelea kutolewa katika jamii bado kuna changamoto kubwa ya jamii kuendelea kuwanyanyapaa watoto hao jambo linalopelekea kukosa haki zao za msingi.
“Tunaomba jamii iwe mstari wa mbele kuwasaidia watoto hawa kutoka kwenye kunyanyapaliwa kwani changamoto hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku na hata kupelekea tatizo kuwa kubwa huku watoto hao wakiendelea kupata shida tunaomba kila mtu kwa nafasi yake ahakikishe watoto hawa wanapata haki zao na kwa wakati kwani wana mahitaji mengi sana .”amesema.
Akizugumzia Mradi wa kuwasaidia Watoto wenye Ulemavu kwa kuzingatia Haki za Binadamu, unaendeshwa kwa ushirikiano na Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Chuo Kikuu Huria Tanzania na Vyuo Vikuu viwili vya Nchini Norway,Mkuu wa chuo cha Ualimu Patandi ,Lucian Segesela amesema ushirikiano na nchi mbalimbali unasaidia kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha watoto wenye ulemavu ambapo umeleta mafanikio makubwa sana kutokana na walimu hao kupata uelewa mkubwa zaidi namna ya kuwahudumia watoto hao.
Amesema kuwa baada ya kujengewa uwezo walimu hao umesaidia sana kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao wa kila siku katika kuyahudumia makundi hayo sambamba na kujifunza mbinu bora zaidi za ufundishaji .
ANITHA KWAYI-Mkufunzi Elimu Maalumu Anitha Kway amesema kuwa , baada ya kupata elimu hiyo itamsaidia sana kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa watoto hao sambamba na kuwa balozi wa kufundisha wengine ambao hawajabahatika na mafunzo hayo.
Utafiti uliofanywa mwaka 2022 na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumiwa watototo UNICEF unaonesha kuwa kati ya watoto milioni 240 wenye ulemavu duniani, nusu hawajawahi kuhudhuria shule, takriban theluthi moja hawapati chakula bora na chakutosha na pia watoto wenye ulemavu wanawakilishwa kwa njia isiyo sawa na wengi wao wanaachwa nyuma.