Na Mwandishi Wetu
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) wilayani Bariadi imejenga Daraja la Mwadobana lenye urefu wa mita 36 na upana mita 9.9 ambalo litachochea ukuaji wa uchumi wilayani humo.
Kaimu Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Khalid Mang’ola amesema hayo wakati wa mahojiano kuhusu miradi iliyotekelezwa na TARURA wilayani humo.
“Tumekamilisha ujenzi wa daraja la Mwadobana, lenye urefu wa mita 36 na upana wa mita 9.9. Daraja hili pamoja na maingilio ya barabara limegharimu shilingi bilioni 1.1, ambapo linaunganisha Kata za Mwaubingi, Nkololo, Banemhi na Mwadobana,” amesema Mhandisi Mang’ola.
Ameendelea kusema kuwa, uwepo wa daraja la Mwadobana utaongeza uchumi wilayani humo, kutokana na biashara za madini ya dhahabu katika Kata ya Mwaubingi, ambapo kwa sasa wafanyabiashara wa madini watakuwa na uhakika na biashara yao kutokana na njia kupitika kwa mwaka mzima bila changamoto yoyote hasa katika kipindi cha masika.
Kwa upande wake Mariam Machibya ambaye ni mkazi wa Kata ya Mwadobana, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa eneo la Mwadobana.
“Tulikuwa tukihangaika namna ya watoto wetu kwenda shule, mto ukijaa watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule, hata sisi wakina mama tulikuwa tukipata shida kwenda kujifungua wakati wa masika, kutokana na mto kujaa maji. Lakini kwa sasa changamoto hizo hazipo tena, kutokana na ujenzi wa daraja hili,” amesema Mariam.
Naye, Malugwi Kamula ameipongeza TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo, ambapo kwake ni kama muujiza kutokana eneo hilo kupoteza maisha ya mke wake na watoto wawili waliosombwa na maji wakati wakivuka eneo lililojengwa daraja la Mwadobana.
“Miaka miwili iliyopita, kabla daraja hili halijajengwa, mto huu ulisomba watu watatu wa nyumbani kwangu, mke wangu, wanangu wawili na baiskeli kwa wakati mmoja. Mke wangu alikuwa na baiskeli na mtoto mgongoni, na mtoto mwingine alikuwa nyuma ya baiskeli,” amesema Kamula.
Aidha, wananchi wa Mwadobana wameishukuru TARURA na serikali kwa ujumla kwa ujenzi wa daraja hilo, ambapo
wameeleza kuwa, kabla ya ujenzi wa daraja hilo watu walikuwa wakisombwa na maji na kupoteza maisha, katika kipindi cha masika, ambapo kwa sasa changamoto haitakuwepo tena, kutokana na ujenzi wa daraja hilo.