Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewapongeza na kuwashukuru Waratibu wa Miradi ya Nishati vijijini kwa uzalendo na juhudi zao zilizowezesha mradi wa kupeleka umeme vijijini kufanikiwa na kukamilika katika ubora uliotarajiwa.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 27, Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wakati wa mazungumzo na waratibu wa nishati vijijini waliopo kila Wilaya ya Tanzania Bara ambapo mikataba yao inatamatika Agosti mwaka huu.
“Safari ya kupeleka umeme katika Vijiji ni kama imekamilika na sasa tumeianza safari ya kupeleka umeme katika Vitongoji. Na nyie mmefanya kazi kubwa sana kufanikisha ndoto ya kufikisha umeme kila kijiji ambayo inaenda kukamilika hivi karibuni kutimia. Na leo tukasema tuje kuwashukuru kwa kazi kubwa mliyoifanya wakati mkitekeleza majukumu yenu kipindi chote cha mkataba cha mwaka mmoja na nusu.
Mmekuwa kiungo muhimu sana baina yetu sisi (REA) na wananchi pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo vijijini. Awali ilikuwa ni vigumu sababu zikitokea changamoto katika miradi, ilikuwa ni lazima wahandisi watoke makao makuu ila uwepo wenu umesaidia changamoto nyingi kushughulikiwa kwa wakati,” amesema Mhandisi Chibulunje.
Amesema kuwa kama Wakala wameomba kibali cha kuongeza mkataba ili waweze kuendelea kutekeleza majukumu ya kusimamia miradi ya nishati vijijini na kuwaomba kuendelea kuwa na wavumulivu huku akiwasisitiza kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa REA.
Kwa niaba ya Waratibu wote, Mratibu wa Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza, Sarah Wambura ameishukuru Serikali pamoja na Wakala kwa fursa waliyopata ya kusimamia miradi ya umeme vijijini na kuomba kama kutatokea fursa zingine basi wasisite kuwaita.