Na Prisca Libaga Arusha.
Serikali imeipongeza Benki ya NMB kwa kuwa moja ya taasisi kubwa ya binafsi inayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi nchini.
Hayo yamesemwa na Afisa Biashara wa Mkoa wa Arusha, Njivaine Mollel kwenye kongamano la Wafanyabiashara ambao ni wateja wa benki ya Nmb lililofanyika jijini Arusha jana Agost 23, 2024.
Amesema kuwa kwa sasa Tanzania imekuwa ikipiga hatua kubwa kwenye maswala ya kiuchumi ambapo imefanikiwa kutokana na mchango mkubwa wa sekta binafsi hasa taasisi za kifedha.
Mollel ameyasema hayo siku chache baada ya Benki kuu ya Tanzania (BOT) kupitia taarifa ya Sera ya Fedha ya Mapitio ya Katikati ya Mwaka 2023/2024, kusema ukuaji wa mapato Tanzania Bara unatarajiwa kufikia takribani asilimia 5.5 mwaka 2024, huku uchumi wa Zanzibar ukitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 7.4.
Mbali na hilo, Benki ya maendeleo ya Afrika (AFDB) imesema kuwa Uchumi wa Tanzania utakuwa zaidi ya asilimia 6.1 hadi mwishoni mwa mwaka huu na kuwa moja ya nchi yenye Uchumi imara Afrika Mashariki.
“Hayo mafanikio yametokana na mchango wa sekta binafsi hasa Mabenki ambao wamekuwa wakitoa fedha zao kuwakopesha wafanyabiashara na wawekezaji kufanikisha shughuli zao”amesema Mollel.
Amesema kuwa mafanikio ya wafanyabiashara kuingiza fedha nyingi kwenye mzunguko inapunguza mahitaji hivyo kukuza uchumi wa nchi.
“Hivyo basi niwapongeze sana Benki ya NMB maana nimesikia hapa wanatoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo hadi Shilingi Milioni 100 ndani ya saa 24 mteja atakapotimiza masharti, kiukweli ni msaada mkubwa kwa serikali yetu kusaidia wananchi wake” amesema Mollel.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wafanyabiashara kukopa fedha iliyo ndani ya mahitaji yao na uwezo wa kulipa ili kuepuka mzigo wa kushidwa kuilipa na matokeo yake kusababisha hasara kwenye biashara zao.
Awali Meneja wa Kanda wa NMB, Baraka Ladislaus amesema kuwa Benki hiyo imekuwa kutoka kukopesha shilingi 200,000 kwa wateja wadogo hadi sasa wanakosha Shilingi million 100 ndani ya saa 24 mteja atakapokidhi vigezo na kutimiza masharti.
Amesema kuwa mbali na hilo pia wana mikopo ya papo kwa hapo ambayo wateja wa benki hiyo wanaweza kukopa kiasi chochote wanachotaka kwa njia ya simu yake hadi shilingi milioni moja kwa simu zao bila masharti wala dhamana yoyote.
“Lengo la kufanya hivi ni kuwaokoa wateja wetu na mikopo umiza ambayo wanakimbilia kutokana na uharaka wake bila kujali riba wala taratibu za kuzilipa, kitendo ambacho imekuwa kilio na mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo ambao wamefikia hadi hatua ya kufilisiwa mali zao” amesema Meneja huyo.
Nae Meneja mwandamizi kitengo cha Biashara, Raynold Tony amesema lengo la kongamano hilo la kila mwaka ni kuwapa wateja wao elimu ya kifedha, bidhaa mpya za benki yao lakini pia kusikiliza changamoto zao za kifedha ili kuzijadili pamoja na kutatua.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wateja kuchangamkia fursa za mikopo ya kibiashara inayotolewa na Benki hiyo na kuhakikisha wanailipa kwa wakati ili iwasaidie kupata sifa za kukopa zaidi kwa ustawi wa biashara zao.
Mmoja wa washiriki wa Kongamano hilo, Anna Sirikwa amesema kuwa Benki ya NMB imekuwa msaada mkubwa kwao hasa elimu ya kifedha na mikopo ambayo imekuwa ikisaidia kukuza biashara zao.