Afisa usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba akifafanua jambo kwa washiriki wa program maalum ya elimu ya fedha iliyofanyika katika Tarafa ya Mikese Mkoa wa Morogoro. Pembeni kwa Bw. Mushumba ni Afisa Mipango kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko na Dhamana (CMSA), Bw. Godfrey Makoi.
Baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Mikese wakifuatilia filamu ya elimu ya fedha iliyotolewa na watalaamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini.
Afisa Mipango kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko na Dhamana (CMSA), Bw. Godfrey Makoi, akielezea namna bora ya uwekezaji kupitia mifuko mballimbali ya uwekezaji nchini katika program ya elimu ya fedha iliyotolewa kwa wananchi wa Tarafa ya Mikese Mkoani Morogoro.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muyanza, akifurahia jambo na mmojawapo wa washiriki aliyehudhuria mafunzo ya elimu ya fedha kwa umma yaliyofanyika Tarafa ya Mikese Mkoani Morogoro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WF, Morogoro)
Na. Ramadhan Kissimba, WF, Morogoro
Wananchi wa Tarafa ya Mikese Mkoani Morogoro wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwapitia elimu ya fedha ambayo inatolewa kupitia Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 – 2029/30.
Wananchi hao walisema kuwa elimu inayotolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini imekuwa na msaada mkubwa katika Tarafa ya Mikese baada ya wananchi wa Kata hiyo kusumbuka kwa muda mrefu kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kutoroka na fedha zao walizokuwa wanawekeza kupitia vikoba visivyo rasmi.
Wakazi hao wameongeza kuwa wamekuwa wakijiunga katika vikundi mbalimbali ili waweze kupata fedha ama kwa kukopa au kwa kujiwekeza, lakini kwa kupitia vikundi hivyo kuna watu ambao sio waaminifu wanatoroka na fedha na kuwafanya wapate hasara jambo linalosababisha kuzorota kwa ukuaji wa uchumi wao.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Fulwe, Kata ya Mikese, Bi. Sarah Stwati, alisema kuwa amekuwa akipokea kesi nyingi kuhusu waweka hazina wa baadhi ya vikundi kuondoka na pesa za wanachama hivyo anaamini kupitia elimu hiyo itakuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Fulwe na Tarafa nzima ya Mikese katika suala zima la uwekezaji.
Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba, alisema kuwa umuhimu wa utoaji elimu kwa wananchi ni kuhakikisha wanaachana na mikopo umiza pamoja na kuwa na uelewa kuhusu taasisi zinazotoa mikopo na vitu vya kuzingatia wakati wa kuchukua mkopo.
Bw. Mushumba aliongeza kuwa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini wanaendesha program ya elimu ya fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali za kufundishia elimu hiyo, ambapo kwa Tarafa ya Mikese wameamua kutumia nyenzo ya filamu ambayo ni rafiki kwa wananchi kwa sababu kupitia filamu wataelimika na kuburudika.
Program ya elimu ya fedha kwa umma inalenga kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga Uchumi na kuondoa umasikini.