Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Wilbrod Mutafungwa, akizungumza na wananchi katika eneo la kivuko cha Kamanga, leo wakiwemo wasafiri, bodaboda na wafanyabiashara wa eneo hilo.


Naibu Meya wa Jiji ambaye pia ni Diwani wa Nyamagana, Bhiku Kotecha, akizungumza na wananchi wakiwemo wasafiri, wafanyabishara na waendesha bodaboda leo, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kamanga Feri, wilayani Nyamagana.

Dereva wa bodaboda, Dominic Domician, anayefanya shughuli zake jirani na kivuko cha Kamanga, akizungumza katika mkutano wa hadhara,leo abapo mgeni rasmi alikuwa Kamanda wa Polisi mkoani humu, Wibrod Mutafungwa.
Picha zote na Baltazar Mashaka.

……….

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
NAIBU Meya wa Jiji la Mwanza na Diwani wa Nyamagana (CCM), Bhiku Kotecha, amewataka wananchi kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi ili kuendeleza ulinzi na usalama katika jiji hilo.
Akizungumza na wafanyabiashara na wasafiri wa kivuko cha Kamanga wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, leo Kotecha amesema jukumu la ulinzi ni la wote na sio la polisi pekee.
“Jukumu la ulinzi ni letu sote. Ikiwa askari mmoja atakuwa na mtu mmoja kati ya wananchi, hali hiyo haitakuwa ya kutosha. Tunapaswa kuwa na mshikamano na kusaidiana ili kujihakikishia usalama wetu,” amesema Kotecha.

Dominic Domisian, dereva bodaboda wa kituo cha Kamanga Feri, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zao katika kuzuia uhalifu, hasa katika usalama barabarani.

DCP Wilbrod Mutafungwa alieleza furaha yake kutokana na imani kubwa ya wananchi kwa Jeshi la Polisi, ametilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kulinda usalama wa mali na watu.

Pia, Kamanda Mutafungwa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la urekebishaji wa kumbukumbu za mpiga kura,huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama wakati wote wa zoezi hilo