Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Daraja la Mto Hurui lililopo katika Kijiji cha Hurui Wilaya ya Kondoa akiwa ziarani mkoani Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na viongozi mbalimbali wakipita katika Daraja jipya la Mto Hurui mara baada kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja hilo lililopo katika Kijiji cha Hurui Wilaya ya Kondoa akiwa ziarani mkoani Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipita katika Daraja la zamani walilotumia wananchi wa Hurui kuvuka katika mto uliopo kijijini kwao mara baada kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja Jipya la Hurui akiwa ziarani Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Hurui mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Daraja la Mto Hurui lililopo katika Kijiji cha Hurui Wilaya ya Kondoa akiwa ziarani mkoani Dodoma
…..
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kufanya ukarabati wa Barabara ya Ntundwa – Hurui ya Wilayani Kondoa ili kuwarahisishisa wananchi shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji mazao.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la mto Hurui lililopo kata ya Kikore Wilaya ya Mpwapwa akiwa ziarani mkoani Dodoma.
Amewahimiza wananchi wa kata ya Kikore na watumiaji wa daraja hilo kutunza miundombinu iliyojengwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye. Amewaagiza kupanda miti maeneo yote pemebezoni mwa mto hurui ili kuokoa daraja hilo lisiharibike kutokana na mmomonyoko wa udongo.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi hao kwa kupata mradi wa daraja uliowaondolea changamoto waliyopata ya kukosa daraja tangu mwaka 2019 lilipoharibiwa na maji daraja la awali. Amewahakikishia wananchi hao serikali itaendelea kuwafikishia wananchi huduma muhimu ikiwemo miundombinu.
Makamu wa Rais akiwa katika kata ya Kikore ameagiza kukamilishwa kwa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata hiyo ifikapo tarehe 30 mwezi Oktoba 2024. Aidha ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini kushughulikia changamoto iliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Hurui kuhusu ardhi ya Kijiji inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji bila kufuata utaratibu.
Ujenzi wa Daraja la Hurui umegharimu shilingi bilioni 1.6 na linatarajiwa kuwa kiungo muhimu na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa kurejesha mawasiliano kati ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Daraja hilo lenye urefu wa Mita 30 limejengwa kwenye barabara ya Ntundwa – Mkunduru -Hurui yenye urefu wa kilometa 46.4. Mradi huo umehusisha uboreshaji wa kilometa 8 za barabara kwa kiwango cha changarawe na umegharamiwa na Serikali kupitia tozo ya mafuta ya shilingi 100.