Na.Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde ameongoza harambee kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania usharika mpya wa Songambele mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, (KKKT) Dayosisi ya kaskazini kati na kupatikana shilingi milioni 53.
Katika ibada ya chagizo iliyoonyozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati Dk Godson Mollel, ambapo Waziri Mavunde alitoa shilingi milioni 10.
Wachimbaji madini ya Tanzanite wengine waliomuunga mkono Waziri Mavunde ni kampuni ya Franone Mining chini ya Mkurugenzi wake Onesmo Mbise, shilingi milioni 15, Chusa Mining chini ya Mkurugenzi wake Joseph Mwakipesile shilingi milioni 12, mkurugenzi wa kampuni ya Gem and Rock Joel Saitoti shilingi milioni 5 na Emmanuel Joseph Wado (Sunda) shilingi milioni 5.
Mbunge wa Afika Mashariki James Ole Millya alitoa shilingi milioni 2, Chama cha mabroka Tanzania (Chamata) shilingi milioni 2 na mdau wa maendeleo Taiko Ole Kulunju alitoa shilingi milioni 1.
Akizungumza kwenye harambee hiyo, Waziri Mavunde amewapongeza wote walioshiriki kwenye uzinduzi wa usharika huo na chagizo la ununuzi wa eneo la Kanisa hilo.
Amewasihi watanzania wawe na utamaduni pia wakushiriki kuchangia shughuli za Mungu na siyo kujihusisha na mambo ya duniani pekee ikiwemo harusi.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel amewasihi waumini wawe na upendo katika maisha yao.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Raphael Lulandala amempongeza Waziri Mavunde kwa kushiriki shughuli za maendeleo kwa siku mbili katika eneo lake.
Mbunge wa Afrika Mashariki James Ole Millya amewapa ushauri KKKT kuomba na kumiliki maeneo mengi hasa ya vijijini kwa manufaa ya miaka ijayo.
Mchungaji kiongozi wa usharika huo Sion Mollel amesema usharika wa Songambele wenye mitaa mitano ulianzishwa Januari mosi mwaka 2023 chini ya mchungaji Loishiye Godson Laizer.
Mchungaji Mollel amesema usharika huo una wakristo 1,357 wakiwemo wanaume 565 na wanawake 792 na umefanikiwa kuwahudumia watu kiroho, kimwili na kiakili.
Amesema lengo lao ni kuishuhudia injili ya Yesu Kristo iletayo wokovu kwa kulihubiri neno la Mungu, kupata chombo cha usafiri ili kurahisisha huduma usharikani.
“Mitaa ya Alamayana na Lengii ipo kilomita 120 kutoka makao makuu ya usharika, kuongeza eneo la makao makuu ya usharika kwa kuwa ni dogo na kuanza ujenzi wa jengo jipya la kuabudia mtaa wa Songambele B,” amesema mchungaji Mollel.