Na mwandishi wetu, Simanjiro
WACHIMBAJI wa madini ya Green Garnet eneo la Lemshuku kata ya Komolo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamelalamikia kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde juu ya changamoto ya ukosefu wa maji, nishati ya umeme na ubovu wa barabara.
Mmoja wa wachimbaji madini ya Green Garnet, mkurugenzi wa kampuni ya Chusa mining LTD, Joseph Mwakipesile ameyasema hayo wakati akizungumza na Waziri wa madini Anthony Mavunde baada ya kutembelea machimbo ya Lemshuku.
Mwakipesile amesema huduma ya maji ni changamoto kwenye machimbo ya Lemshuku na hakuna nishati ya umeme hivyo kushindwa kufanya uchimbaji kwa uhakika.
“Maji yanafuatwa umbali wa kilomita 17 kutoka kijiji cha Komolo Hadi hapa machimboni na tulikuwa na kisima cha maji ila hivi sasa tuna maji tunafuata mbali na pia barabara ni mbovu,” amesema Mwakipesile.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini (MAREMA) Tawi la Lemshuku, Swalehe Abdalah ameiomba serikali kufanikisha changamoto hizo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji kwa uhakika.
“Tunakushukuru Waziri Mavunde kwa kufika Lemshuku na kuona mazingira ya hapa Lemshuku tunaomba serikali imalize vikwazo tulivyonavyo ili tufanye kazi vyema,” amesema Swalehe.
Hata hivyo, Waziri Mavunde amesema atakutana na Mawaziri husika ili kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi ili wachimbaji hao waweze kufanya kazi zao ipasavyo na Serikali iongeze mapato.
Waziri Mavunde amesema miundombinu ikiboreshwa na changamoto zikipatiwa ufumbuzi watanzania hao watatajirika kwa kupata fedha nyingi na serikali itaongeza mapato kupitia kodi.
Hata hivyo, ili kumaliza changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya ameendesha harambee ya ghafla ya ujenzi wa zahanati na kupatikana Sh23 milioni matofali 3,000 na mifuko 185 ya saruji
“Nanyi wachimbaji mtatumia nguvu kazi kwa kuchimba msingi, kukusanya mawe na mchanga ili ujenzi uanze mara moja kwa kutumia matofali na saruji zilizopatilana,” amesema Waziri Mavunde.
Ameuagiza uongozi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro kuhakikisha pampu iliyozama kisima cha maji Lembole inatolewa ili wachimbaji wapate huduma wakisubiri mradi mkubwa wa maji.
“Mkuu wa wilaya ya Simanjiro kaka yangu Fakii Lulandala ataweza kusimamia suala la ukarabati wa barabara kwa kuagiza wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) kutengeneza barabara ili muweze kupita kwa urahisi,” amesema.
Akizungumza juu ya mawasiliano amesema atazungumza na waziri husika ili mnara wa simu ufungwe kwenye machimbo hayo na mawasiliano yapatikane.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala amesema hii ni mara ya kwanza Waziri wa madini kufika kwenye machimbo ya Lemshuku hivyo Waziri Mavunde anapaswa kupongezwa.
“Umeandika historia kwa kuwa Waziri wa madini wa kwanza kufika kwenye machimbo ya Green Garnet eneo la Lemshuku na umetembelea migodi mitatu na kuzungumza na wachimbaji wa madini” amesema Lulandala.
Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini Femata John Bina amesema Waziri Mavunde ni kiongozi wa pori kwa pori asiyekaa ofisini ndiyo sababu amefika Lemshuku.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Ormemei Laizer amesema mahitaji ya binadamu ni endelevu hivyo wachimbaji hao mahitaji yao yanapaswa kukidhiwa waweze kufanya kazi zao vyema.
Mwenyekiti wa chama cha mabroka Tanzania (Chamata) Jeremiah Kituyo amewaasa wanunuzi wa madini kukata leseni ili waweze kuwa huru na biashara yao.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amesema wachimbaji hao wa Lemshuku wakitatuliwa changamoto zao watanufaika ikiwemo wachekechaji.