NA FAUZIA MUSSA

TAASISI ya ‘Together for Samia’ imesema inaendelea na mikakati  ya kuelezea  utendaji kazi wa viongozi wakuu wa Nchi ili jamii itambue na kuthamini juhudi za viongozi hao.

Mwazilishi wa Taasisi ya hiyo  Slim Salim Mohammed ameyasema hayo katika hafla  ya kutoa ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dk. Samia Suluh Hassan kwa njia ya makachu huko Forodhani Mjini Unguja.

Alisema utendaji kazi wa kiongozi huyo unamgusa kila mtu wakiwemo vijana , jambo ambalo alilitaja kuwasukuma  kuanzisha taasisi hiyo ili kuzielezea  juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi kwa jamii, Taifa na Dunia kwa ujumla.

 “Dk. Samia anafanya vizuri katika Sekta  zote, ikiwemo  afya, elimu, miundombinu na hata demokrasia jambo ambalo linaleta Amani katika  Nchi yetu.” alisema Slim

Aidha alieleza kuwa Taasisi hiyo imeamua kuwatumia Vijana wa makachu kufanikisha hafla hiyo  ili ujumbe unaotolewa kufika kwa  wananchi wa Tanzania na dunia kwa ujumla kwa haraka zaidi.

Vilevile alisema hivi karibuni Taasisi hiyo itazielezea na kuonesha shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ikiwa ni sehemu ya kutambua jitahada anazozichukua kiongozi huyo katika  kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo vijana.

Miongoni  mwa wananchi walioshuhudia hafla hiyo Massoud Salim Mohammed alisema hatua ya vijana hao kuanzisha na kuendesha  taasisi hiyo kwa gharama zao kunaonesha wazi mapenzi waliyonayo kwa viongozi wa nchi  pamoja na kuthamini juhudi za kimaendeleo za viongozi hao.

Alieleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na viongozi makini, na mahiri wenye mapenzi na wanachi wao  waliojitoa kuendesha nchi bila kujali maslahi binafsi, hivyo kuna kila sababu ya watanzania kutambua na kuthamini juhudi hizo.

Kwa upande wake Mwazilishi wa Makachu Jamal Amour Abdalla alisema wanafurahishwa kuona Sanaa yao inaendelea kutumika katika kufikisha ujumbe wa matukio mbalimbali ya kitaifa  na kimataifa.

Aidha  aliziomba Serikali zote mbili kuwasaidia wasanii hao  kupata bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu  wakati wote.

Hatahivyo  waliomba Serikali na wadau wa Sanaa hiyo kuweka kituo cha  huduma za dharura katika  eneo wanaloendeshea shuguli zao  pamoja   na gari la kubebea wagonjwa ili kusaidia kuwahi kituo cha afya pale madhara yanapotokea.

Miongoni mwa ujumbe uliotolewa na vijana wa ‘together for Sami’ kwa njia ya makachu ni pamoja na “mama tunakupenda, tunakuthamini na tutakulinda, muumini wa maridhiano, kipenzi cha wengi, anaimarisha uchumi na kuipaisha Tanazania siku hadi siku , Mjenzi wa Demokrasia.”