Na Mwamvua Mwinyi
Mama lishe na baba Lishe zaidi ya 70 katika Wilaya ya Kibaha ,Mkoani Pwani ,
wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka Kampuni ya INTERFINi kwa ushirikiano wa Maestro Afrika na kudhaminiwa na Benki ya CRDB
Baada ya Kibaha,mafunzo hayo yanalenga kuwafikia mama lishe na baba lishe 5,000 ifikapo 2026 .
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon aliipongeza Kampuni ya INTERFINi kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Nickson alibainisha kuwa, jamii inapaswa kudadilika kuona umuhimu wa kutumia nishati mbadala na safi kwa manufaa yao.
Awali Meneja mradi wa Kampuni ya INTERFINi Pamela Mushi alieleza, mafunzo hayo yamelenga kupata uelewa juu ya matumizi ya nishati safi kupitia program ya mapishi hodari kwa mama na baba lishe wapatao 70 iliyoandaliwa na Kampuni ya INTERFINi kwa ushirikiano na Maestro Africa Solutions Kwa ufadhili wa benk ya CRDB.
Alieleza, wanafanya kazi na Serikali, Mashirika Binafsi na Kimataifa na wamefanyakazi katika sekta ya nishati kwa miaka kumi hususan maeneo ya Vijijini.
“Katika kuona tatizo la nishati isiyo mbadala tukaona umuhimu wa kuanzisha program ya mpishi hodari ili kusaidia jamii kuongeza ulewa wa manufaa ya nishati safi ya kupikia,ili watu wabadilishe mtazamo katika nishati safi ya kupikia, kuacha kutumia kuni na mkaa”
“Mtu akitumia kuni na mkaa wanatumia muda mrefu,tunaangalia gharama bila kuangalia muda, lakini tumeona kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa vitendo kuona namna gani ya kutumia nishati safi”.
“Kwa kuzingatia hili tumetoa mafunzo kwa baba na mama lishe kwakuwa wanatumia muda mrefu kukaa kwenye jiko,moshi,moto dhana kubwa wapate uelewa na tunajikita pia zaidi maeneo ya vijijini.”alifafanua Pamela.
Kadhalika Pamela alieleza, lengo jingine la program ya mpishi hodari ni kutunza mazingira na kusisitiza kuwa matumizi ya nishati safi siyo anasa.
Akielezea kuanza kwa mpango huo anasema walianza 2023 na wanatarajia kufika Zanzibar, Dodoma ,Pwani, Morogoro ili kuendelea kutoa mafunzo na elimu hiyo.
Mama lishe Ashura Kituta alieleza , wanatarajia mafunzo hayo yataleta matokeo chanya katika shughuli zao za kila siku na kushukuru kuwa miongoni mwa waliopata mafunzo hayo.
Rose Kazimoto, Meneja Benk ya CRDB Tawi la Kibaha alieleza, Taasisi hiyo inashirikiana na jamii na ipo pamoja na Serikali kupambana na matumizi ya nishati isiyo salama kwa afya za binadamu.