KAIMU Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bi. Irene Gowelle akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 19,2024 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya maboresho ya mfumo wa Luku unaotarajiwa kuanza Agosti 26,2024.
Na.Alex Sonna-DODOMA.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataka wateja wake wa Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini kufanya maboresho ya mfumo wa Mita za Luku ikiwa na lengo la kuendana na mabadiliko ya mfumo wa mita hizo Kimataifa pamoja na kuongeza ufanisi na usalama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 19,2024 jijini Dodoma,Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma TANESCO Bi. Irene Gowelle,amesema kuwa zoezi la maboresho ya mfumo wa Luku ambalo litaanza rasmi Agost 26,2024 katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida,Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Amesema kuwa maboresho ya luku yatafanyika kuanzia Agosti 26,2024 wakati mteja atakaponunua umeme kwa mara ya kwanza na kupokea tarakimu kwenye makundi matatu ambapo kila kundi litakuwa na tarakimu 20.
Bi. Gowelle amesema kuwa kundi la kwanza na pili la tarakimu litakuwa kwa ajili ya maboresho ya mfumo wa luku, huku kundi la tatu kwa ajili ya umeme utakaokuwa umenunuliwa na mteja.
“Mteja ataingiza umeme tarakimu za kila kundi katika luku yake kwa mfatano unaosomeka kwenye risiti ya malipo au ujumbe mfupi wa maandishi (sms) na kila utakapoingiza kundi moja mteja anapaswa kubonyeza alama ya kukubali ya # au msale wa kukubali na hapo utakuwa umefanikiwa kuboresha mita yako na kupokea kiwango cha umeme ulionunua” amesema Bi. Gowelle.
Bi. Gowelle amesema kuwa TANESCO wajipanga katika mikoa yote kwa ajili ya kuwasaidia wateja wakati wanapopata na changamoto katika kipindi chote cha maboresho ya mita za luku.
“Zoezi la maboresho ya luku ni bure na litafanyika mara moja kwa kila mteja na baada ya kufanya hivyo atakuwa amefanya maboresho na ataendelea kupata kundi moja la tarakimu 20 kila atakapofanya manunuzi ya umeme” amesema Bi. Gowelle.
Aidha ameeleza mafanikio kwa kanda na mikoa ambayo zoezi lilikuwa limeshaanza ,tumefanikiwa kuwawezesha wateja asilimia 84 kuweza kufanya maboresho ya mfumo wa Luku, kwahiyo mnaweza kuona hizi asilimia zilibaki ni za mikoa ambayo tulikuwa hatujaingia, na hii imetokana na muitikio mzuri wa wateja kwa matangazo tuliyokuwa tunayatoa na wao kuyafuatulia vizuri kulipelekea kurahisha zoezi hili”.
Shirika linawahimiza wateja wake wote kuendelea kununua umeme ili kuweza kufanya maboresho hayo kwenye mita zao ambapo ukomo wa zoezi hilo katika maeneo yote ya nchi nzima utakuwa tarehe 24/11/2024.