Na Prisca Libaga Arusha
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini tarehe 18.08.2024 imetoa elimu kinga kwa waumini wa dini ya kikristo zaidi ya 250 katika Kanisa la Kikatoliki Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga USA River katika Wilaya ya Arumeru mkoani wa Arusha.
Kauli na elimu hiyo imetolewa na Shabani Miraji ambaye ni Afisa Elimu Jamii wa DCEA Kanda ya Kaskazini ambapo alieleza dhamira ya Mamlaka ya kutoa elimu hiyo katika nyumba za ibada za imani mbalimbali katika Mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini.
Waumini walioshiriki ibada kanisani hapo waliaswa kutojihusisha na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kutimiza ndoto zao za mafanikio ya baadaye lakini pia walihimizwa juu ya kutowanyanyapa waraibu wa dawa hizo na badala yake wawaunganishe waraibu hao katika Vituo vya huduma za matibabu zilizopo karibu na mazingira yao wanayoishi.
Ofisi Kanda ya Kaskazini ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii zikiwemo nyumba za ibada za imani zote ili kuhakikisha kila kundi linafikiwa katika maeneo yote ya Kanda ya Kaskazini.