Afisa Kilimo Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Kanda ya Magharibi Bluma Kalidushi akizungumza juu ya zao la pamba .
Mmoja ya Shamba Darasa la zao la pamba
Na Lucas Raphael,Tabora
WAKULIMA wa zao la pamba nchini wametakiwa kufanya kilimo chenye tija na kuhakikisha wanafuata kanuni, taratibu na maelekezo ya wataalamu wakati wa kuandaa mashamba, ukuzaji na wakati wa kuvuna.
Rai hiyo imetolewa jana na Afisa Kilimo Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Kanda ya Magharibi Bluma Kalidushi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mkoani hapa .
Alieleza kuwa kilimo chenye tija kina manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwa kinaongeza uzalishaji na kumwezesha mkulima kupata mazao bora ambayo huvutia soko hivyo kununuliwa kwa bei ya juu.
Alibainisha kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa hawazingatii maelekezo ya wataalamu kuanzia mwanzo na wakati wa uvunaji hali inayopelekea baadhi yao kuweka takataka wakati wa kuvuna hivyo kuwasababishia hasara.
Kalidushi alifafanua kuwa hali hiyo hupelekea kuharibika kwa mitambo ya kuchambua pamba na matokeo yake kuongeza gharama za uchambuaji kwenye mitambo hiyo (Jineri).
Aidha aliongeza kuwa baadhi yao wanaongeza vitu visivyotakiwa ikiwemo maji na mchanga hivyo kusababisha makampuni wanayofanya nayo biashara kuwatoza gharama kubwa za ukarabati wa mitambo punde inapoharibika mara kwa mara.
Kalidushi alisema kuwa madhara ya kuweka mchanga kwenye pamba baada ya kuvunwa inaharibu mitambo, kwa kuwa haihitaji kusaga kitu kigumu.
‘Dira ya Bodi ya Pamba ni kuongeza uzalishaji na kukuza ushindani katika tasnia ya kilimo cha zao hilo hapa nchini ili kumnufaisha zaidi mkulima na sio vinginevyo’, alisema.
Alibainisha kuwa zao hilo hadi sasa linalimwa katika jumla ya Mikoa 17 iliyoko katika Kanda ya Magharibi na Kanda ya Mashariki na limeendelea kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa wakulima.
Kadushi waliongeza kuwa zao hilo linaweza kulimwa katika maeneo yote ili mradi kuwe na ardhi yenye rutuba nzuri na mvua za wastani zinazoweza kuchochea uzalishaji mkubwa.
Alitoa wito kwa wahusika wanaopokea zao hilo kutoka kwa wakulima baada ya kuvunwa kuhakikisha inakuwa na ubora na viwango vinavyotakiwa ili kuwarahishia soko na kuuza kwa bei nzuri.