Na. Mwandishi wetu – Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya Watu Wenye Ulemavu ikiwemo kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa wenye Ulemavu.
Aidha, amesema mkakati mwingine ni kukamilisha mwongozo wa ufikivu ambao utaondoa vikwazo vya upatikanaji wa huduma kwa Watu wenye Ulemavu.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo leo Agosti 15, 2024 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa semina ya kuwajengea uelewa wajumbe wa baraza la taifa la ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu kuhusu mfumo wa kielektroniki wa taarifa na kanzidata kwa wenye Ulemavu, ujumuishwaji wa anuai za jamii katika mradi wa Tanzania ya kidijitali na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia saidizi (2024 – 2027).
Vile vile, Mhe. Ridhiwani amesema serikali itaendelea kutoa elimu na kusambaza mwongozo wa uimalishwaji, uendeshaji na ujumuishwaji wa huduma kwa watu hao, kusambaza mfumo wa kielektroniki wa taarifa , kanzidata wa Watu wenye Ulemavu na kuwajengea uwezo watoa huduma wa afya, elimu, ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii katika kutambua mapema watoto wenye Ulemavu.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wajumbe wa baraza hilo kuendelea kutejkeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi mapana ya watu wenye ulemavu ikiwemo kushauri kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino.
Akizungumza awali, Naibu Katibu Mkuu Ofisi hiyo Bi. Zuhura Yunus amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imeendela kutoa msisitizo kuhusu asilimia 3 ya ajira kwa Watu wenye Ulemavu ili wanufaike na fursa hiyo.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu wenye Ulemavu Dkt. Lucas Kija amesema baraza hilo litaendelea kuishauri serikali ili kuleta usawa katika masuala ya ajira, afya, elimu, miundombino na teknolojia.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza hilo, Bi. Johari Iddy, ameishukuru serikali kwa kuanzisha baraza hilo, ambalo linawapa fursa ya kutoa maoni na ushauri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Watu wenye Ulemavu.
Baraza la Ushauri la Taifa la Watu wenye Ulemavu limeundwa kwa mujibu wa sheria Na. 9 ya mwaka 2010.