Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda akizungumza kwenye baraza la madiwani halmashauri ya Arusha .
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, Dkt. Ojung’u Salekwa akizungumza na madiwani hao mkoani Arusha.
Happy Lazaro ,Arusha .
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda, amewataka madiwani kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha na kupiga kura kuchagua Wenyeviti wa vijiji.
Kaganda ameyasema hayo wakati akizungumza katika baraza la madiwani wa halmashauri ya Arusha DC na kuwakumbusha wajibu wao wa kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi .
Amesema kuwa, katika madiwani ndio usimamizi mwananchi katika maeneo yao hivyo ni wajibu wao kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anatoa elimu kwa wananchi ili waweze ufahamu wajibu wao katika kuchagua viongozi wanaowahitaji.
“Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan, ametuma fedha nyingi za miradi ya maendeleo, hivyo ni jukumu la madiwani kuzisimamia kwa umakini zaidi ili miradi hiyo itekelezwe kwa ubora na ikamilike kwa wakati.”amesema Kaganda.
Aidha Kaganda aliwaasa madiwani kwenda kwa wananchi na kuwaeleza miradi inayotekelezwa na serikali kwani ni wajibu wao kwenda kwa wananchi kuwaeleza miradi inayotekelezwa na serikali na wao kama wenyeviti wa kamati za maendeleo ya kata wakasimamie kuhakikisha watendaji na wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanaeleza wananchi miradi inayotekelezwa ili ikamilike kwa ukamilifu na wakati,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, Dkt. Ojung’u Salekwa, amewataka wananchi wa halmashauri hiyo kuwa na amani na kuwahakikishia kuwa zaidi ya shilingi milioni 600 zilizokuwa zimepotea zimesharudi zote.
Dkt. Salekwa amesema kuwa fedha hizo zilipotea kwenye baadhi ya taasisi za kifedha na watumishi wawili wa halmashauri, lakini baada ya uchunguzi, taasisi hizo zilijiridhisha na kurejesha fedha zote.
“Mimi kama mwenyekiti wa halmashauri niseme kuwa fedha hizo zilipotea kwenye baadhi ya taasisi za kifedha na watumishi wawili wa halmashauri na taasisi hizo baada ya kujiridhisha kuna makosa yalifanyika kwa upande wao walisharudisha fedha hizo zote zimesharudi na moja kwa moja zitaenda kwenye vituo vya afya na zahanati ambazo upotevu huo ulitokea,” amesema Dkt. Salekwa.
Aidha kwenye kikao hicho, madiwani walijadili suala la taarifa zilizokuwa zikizagaa kuwa halmashauri hiyo ilikuwa na bakaa ya shilingi bilioni 8.5.
Ambapo kuhusiana na taarifa hizo Dkt. Salekwa amesema, “Taarifa sahihi mpaka tunafika mwisho wa mwaka Juni 2024, fedha ambazo zilikuwa hazijatumika ni kama bilioni 2.7 ambazo zilikuwa na maelezo kwani zilikuwa ni za miradi mikubwa iliyokuwa inaendelea na haijakamilika kama Olturmet wenye zaidi ya shilingi milioni 900 na shule kama Engalaon.”
Hata hivyo Dkt. Salekwa amewapongeza madiwani kwa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kusimamia fedha zinazoletwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kama ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa.