Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia wa mali zao kwa kufanya doria na misako pamoja na kutoa elimu ya Polisi Jamii hali iliyopelekea kupata mafanikio katika kuzuia na kupambana na uhalifu. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2024 jumla ya watuhumiwa 602 wa makosa ya mauaji, kujeruhi, wizi, kupatikana na silaha bila kibali, pombe moshi, bhangi na uvunjaji wa nyumba walikamatwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia Sebastian Thomas [37] Dereva, Mkazi wa Isanga Jijini Mbeya na Silvester Mashaka Mashauri [40] Mkazi wa Iganzo Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na silaha bunduki aina ya Shotgun yenye namba za usajili C328809 bila kuwa na kibali cha umiliki wa silaha hiyo.
Mtuhumiwa Sebastian Thomas [37] alikamatwa akiwa na silaha hiyo akiwa ameificha kwenye mfuko wa sandarusi na kuiweka nyuma ya kiti cha Dereva ndani ya Gari namba T.844 DME Tata inayosafirisha abiria kati ya Mbeya kwenda Chunya.
Mtuhumiwa baada ya kukamatwa alieleza kupewa silaha hiyo na mtuhumiwa Silvester Mashaka Mashauri kwa ajili ya kwenda kutumika katika shughuli za ulinzi machimboni katika kampuni binafsi.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Lugano Tutufye [29] Mkazi wa RRM Ilomba Jijini Mbeya kwa tuhuma ya kupatikana na silaha ya wizi Bastola aina ya Browing ikiwa na risasi zake 9 ndani ya magazine mali ya Said Mussa Mwatuka [46] Mkazi wa Chamanzi Dar es Salaam.
Awali Agosti 04, 2024 eneo la PM Hotel lililopo Nanenane Jijini Mbeya Said Mussa Mwatuka [46] aliibiwa Silaha Bastola iliyokuwa ndani ya Gari lake aina ya Subaru Impleza rangi nyekundu yenye namba za usajili T.410 DYB baada ya mtuhumiwa ambaye alimpakiza kama abiria kuiba silaha hiyo na kuondoka nayo.
Ufuatiliaji ulifanyika na Agosti 05, 2024 huko maeneo ya Nanenane Jijini Mbeya mtuhumiwa alikamatwa akiwa na silaha hiyo na risasi zake ndani ya magazine. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani.
Aidha, katika kukabiliana na uingizaji wa bidhaa za magendo nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kuingiza nchini sukari kwa njia ya magendo. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa bodi ya sukari nchini liliendesha oparesheni ya pamoja Julai 25, 2024 na kukamata kiasi cha kilogramu 420 za sukari zilizoingizwa nchini bila kibali kutoka nchini jirani ya Malawi na Zambia.
Watuhumiwa waliokamatwa katika oparesheni hiyo ni 1. Oria Mwakaselema [48] Mkazi wa Mwakibete, 2. Anyosisye Mwambona [63] Mkazi wa Ilomba, 3. Fredy Nyangalima [57] Mkazi wa Uwanja wa Ndege wa Zamani, 4. Itika Mwanyula [28] Mkazi wa Forest na 5. Jenny Seme [52] Mkazi wa Isyesye Jijini Mbeya.
Sambamba na hayo, katika kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani kwa kipindi cha mwezi Julai, 2024 jumla ya makosa ya barabarani 8968 yalikamatwa kati ya hayo magari 7149 na Pikipiki/Bajaji 1819. Pia jumla ya madereva 26 walifikishwa mahakamani kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani kwa kuendesha vyombo vya moto kwa uzembe na kuhatarisha maisha ya watumiaji wengine wa Barabara, Dereva 1 amefungiwa leseni yake ya udereva.
Vile vile, katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kipindi cha mwezi Julai, 2024 jumla ya watuhumiwa 23 walikamatwa kwa makosa ya kupatikana, kuuza, kutumia na kusambaza dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilo 15 na Gram 368 ilikamatwa.
Pia kwa kipindi cha mwezi Julai, 2024 jumla ya kesi 844 zilifikishwa mahakamani ambapo kesi 159 zilipata mafanikio kwa watuhumiwa kukutwa na hatia na kuhukumiwa vifungo jela ikiwemo kifungo cha maisha na miaka thelathini jela. Kesi 685 zipo katika hatua mbalimbali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa wananchi kutofumbia macho uhalifu kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za viashiria vya uhalifu ili hatua stahiki zichukuliwe. Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa madereva wa vyombo vya moto kufuata sheria na kuheshimu watumiaji wengine wa barabara ili kuepuka ajali.
Imetolewa na:
Benjamin Kuzaga – SACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.