Na Mwandishi wetu, Arusha
WAKULIMA nchini wanaolima mazao na kuongoza kwa lishe duni hadi kusababisha watoto wao kupata udumavu wametakiwa kubadilika kwa kujijali na kula vyakula hivyo na siyo kuviuza pekee.
Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Manyara, Fakii Raphael Lulandala ameyasema hayo Agosti mosi kwenye ufunguzi wa maonyesho ya 30 ya kilimo na sherehe za nane nane kanda ya kaskazini kwenye viwanja vya Themi Njiro jijini Arusha.
Lulandala ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Simanjiro, amesema wakulima wanaolima mazao na kuacha kutumia hadi watoto wao wanakuwa na udumavu wanafanya makosa makubwa.
“Nashangazwa na mikoa inayoongoza kwa kilimo nchini ikiwemo ya Njombe, Iringa na Manyara ila baadhi ya jamii yake inapata lishe ndogo na kusababisha udumavu usiokuwa na lazima,” amesema Lulandala.
Amesema wakulima hao wanapaswa kula vyakula bora wanavyoelezwa na wataalamu wa lishe kuliko kulima na kuuza mazao yao hivyo kusababisha udumavu.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ambaye ni Kaimu mkuu wa mkoa wa Arusha, amesema maonyesho hayo yana manufaa makubwa kwani elimu ya kilimo, mifugo na uvuvi inatolewa kwa washiriki.
“Maonyesho haya yanashirikisha mikoa mitatu ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, hivyo watu washiriki kwa wingi kwani yatafunguliwa rasmi Agosti 3 na kufungwa Agosti 8,” amesema Babu.
Amesema wakulima wakishiriki maonyesho hayo wanajifunza mambo mengi kupitia mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yaliyopo.
“Watauliza maswali kwa wataalamu wetu wa kilimo, mifugo na uvuvi na kujionea kwa macho kupitia maonyesho hayo ambayo yatafanyika kwa muda wa siku nane,” amesema Babu.
Mmoja kati ya wakulima aliyeshiriki maonyesho hayo Mwinyijuma Ismail kutoka kijiji cha Lengatei wilayani Kiteto, amesema kupitia maonyesho hayo atajifunza ufugaji na ukulima wa kitaalam.
“Wataalamu wa kilimo na mifugo wapo hapa ambapo nitajifunza namna ya kulima na kufuga kitaalam na kupata mazao mengi zaidi tofauti na awali,” amesema Ismail.
Amesema amejifunza namna zao la muhogo aina ya kiroba kutoka kata ya Mutuka wilayani Babati ambapo miche 4,000 inapandwa kwenye ekari moja na kupata tani 40.
Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu wa 2014 ni chagua viongozi wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi