Tawi la Pamba Jiji FC lililofunguliwa Buchosa
Wananchi waliojitikeza kwenye ufunguzi wa Tawi la Pamba Jiji FC Buchosa
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya siku inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Jijini Mwanza,Pamba Day,kampeni yake imezidi kuwabamba mashabiki baada ya kufunguliwa tawi jipya huko Buchosa wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Tawi hilo la mashabiki wa Pamba Jiji FC limefunguliwa Jana Agosti 1, 2024 na katibu Tarafa wa kata ya Kahunda,Joseph Kapunda kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo na kusisitiza huo ni muendelezo wa kufunguliwa matawi zaidi wilayani humo.
“Tuna wajibu wa kushikamana kwa vitendo kuiunga mkono timu yetu ya Pamba Jiji FC ambayo mbali na burudani imekuja kuinua uchumi wa mkoa wetu,”Kapunda.
Amesema siku ya Pamba Day itadhihirisha furaha ya mashabiki kwa timu yao kwa kuujaza kwa wingi uwaja wa CCM Kirumba na mechi zote za ligi kuu ya NBC.
“Tulimsikia Mkuu wetu wa Mkoa Mhe Said Mtanda akituhimiza kushikamana na tuwe wachezaji wa 12 uwanjani siku zote za michuano ya timu ya Pamba Jiji akimaanisha kuishabikia uwanjani”,amesisitiza katibu Tarafa wakati akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa tawi la mashabiki wa Pamba Jiji FC.
Mwenyekiti mteule wa tawi hilo Salawe Magembe amebainisha atahakikisha kwa kushirikiana na wanachama wenzake wanazidi kuliimarisha tawi hilo na kuwa wakereketwa wa kweli kwa timu ya Pamba Jiji FC.
Mchezaji wa zamani wa Pamba miaka ya 90 ambaye alikuwa mlinda mlango Madata Lubigisa amewataka mashabiki wa soka kuhakikisha timu yao inadumu katika ligi hiyo na kuwa tishio kwa timu za uzito wa juu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Nimefurahi mlivyo hamasika na timu yenu ya Wana Kawekamo TP Lindanda,Pamba Jiji FC ufunguzi wa tawi hili uwe msingi bora wa kupanga mikakati mbalimbali ya kuipa maendeleo timu yenu,”Agnes Magubu,kiongozi wa Kampeni ya Pamba Day
Kampeni hiyo inayoendelea kwenye wilaya zote za Mkoa wa Mwanza inakwenda Pamoja na uuzwaji wa tiketi za kuingilia siku ya Pamba Day na jezi za timu hiyo.