WAKAZI wa Mkoa wa Dodoma wanatarajiwa kushuhudia tukio la uzinduzi rasmi wa safari za treni ya kisasa ya (SGR) utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, Agosti mosi mwaka huu katika Stesheni ya mkoa wa Dodoma.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma,Bi. Rosemary Senyamule,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandilizi ya mkoa kufanikisha tukio hilo la kihistoria.
RC Senyamule amesema kuwa maandalizi yote kwa asilimia kubwa yamekamilika hivyo wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na ile ya jirani hawana budi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo la kihistoria.
“Mkoa wa Dodoma umepewa heshima kubwa ya kuandaa tukio hili la kihistoria ambalo kila mmoja wetu anapaswa kushiriki kwani haliwezi jirudia tena”amesema RC Senyamule
Akizungumzia kuhusu kuanza kwa safari za treni kutoka Dar es Saalam hadi Dodoma amesema kuwa kutasaidia kuufungua mkoa wa Dodoma kiuchumi kwakuwa wafanyabiashara wengi watatumia usafiri huu kupunguza muda wa kufuata bidhaa zao.
“Usafiri huu unakwenda kupunguza muda wa safari ambao watu walikuwa wakitumia hapo awali hivyo mfanyabiasahra atakuwa na uwezo wa kwenda Dar asubuhi na kurudi jioni akiwa na bidhaa zake tayari”amesema
Aidha ameipongeza serikali kwa kufanikisha kukamilisha ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati ambao utakwenda kuongeza shughuli za kiuchumi na kukuza kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Safari ya kwanza ya treni ya kisasa ya umeme (SGR) kutoka Dar es Saalam kwenda Dodoma ilianza rasmi Julai 25, mwaka huu huku abiria zaidi ya 1000 wakitumia usafiri huo na wengine kukosa nafasi.
Hata hivyo amewataka Maafisa usafirishaji Mkoa wa Dodoma kutumia vyema fursa ya ujio wa treni ya kisasa kwa kuhakikisha wanalinda picha ya Serikali kwa kuwafikisha salama abiria watakao kuwa wanatumia treni hiyo.