MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amefanya ziara katika Kata ya Kikio na kukagua mradi wa maji wa kijiji cha Mkunguwakihendo na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.9 kwa ajili ya miradi ya maji kwenye jimbo hilo.
Ili jitihada za Rais Dkt Samia za kumtua mama ndoo ya maji kichwani zifanikiwe amemtaka Meneja wa RUWASA wilaya ya Ikungi kuongeza nguvu kazi ili mradi wa maji wa Mkunguwakihendo ukamilike ndani ya miezi miwili kuanzia sasa na Septemba 2024 wananchi waanze kunywa maji waliyoyasubiri kwa muda mrefu.
Mtaturu ametoa shukrani hizo Julai 29,2024,akiwa kwenye ziara katika Kata ya Kikio kwa ajili ya kutoa mrejesho wa Bunge la Bajeti 2024/2025,kuhamasisha uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji 2024 na kusikiliza kero za wananchi.
“Mradi huu umechelewa kukamilika kwa sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni Mkandarasi aliyepewa kazi alisuasua akaondolewa na kuamuliwa ujenzi usimamiwe na Ruwasa kwa kutumia mfumo wa Force Account, kwa sasa kazi za kujenga Pump house imekamilika,utandazaji wa mabomba kwenye DPs umekamilika ikiwemo bomba kutoka chanzo cha maji hadi kwenye tanki,”.amesema.
Amesema ujenzi wa tanki unaendelea upo asilimia 25 na matarajio ni mradi ukamilike disemba 2024 ambapo kukamilika kwake kutaondoa adha ya wananchi kwenda kutafuta maji umbali mrefu.
“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji kwenye jimbo la Singida Mashariki inayofikia Shilingi Bilioni 1.9,”amesema.
Meneja wa RUWASA Ikungi akisoma taarifa ya mradi huo amesema ni mradi mmojawapo kati ya miradi mingi inayotekelezwa kwenye jimbo la Singida Mashariki ambapo serikali ilitenga Shilingi Milioni 312 ili kutekeleza mradi huo.
Diwani Wa Kikio Kalebi Nkhondeya amempongeaza Mbunge Mtaturu kwa kupaza sauti bungeni na serikali kuleta fedha za miradi mingi kwenye Kata yao hususan katika sekta ya Elimu,Umeme,Maji na Miundombinu ya barabara.