MAENDELEO waliyoletewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,wananchi wa Magu wamwoneshe fadhila kwa kumpigia kura za heshima mwakani,wakianzia na uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo kwa nyakati tofauti na Mbunge wa Magu, Bonventure Kiswaga,Mwenyekiti wa CCM, Enos Kalambo na Katibu wa Chama wa Wilaya hiyo, Fratha Katumwa wakati wakihutubia mikutano ya hadhara katika vijiji vya Kitumba, Igekemaja, Buseka na Kanyama.
Kiswaga alisema yeye,madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa ni chombo cha kubeba kero na changamoto za wananchi na kuzifikisha panapo husika kwa utatuzi hatimaye wapate maendeleo.
Kiswaga amesema changamoto za maji na umeme zimesababishwa na ongezeko la watu na hivyo serikali inajitahidi kuzitatua kwa kuwafikishia wananchi huduma hizo ingawa haiwezi kuzitatua zote kwa wakati mmoja.
“Hakuna jambo gumu kama elimu na naomba mtuamini,serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha maendeleo yanapatikana,suala la uhaba wa madawati wananchi wanachangie,tuwanusuru watoto na adha ya kukaa chini,”amesema mbunge huyo wa Magu.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya,Enos Kalambo amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu 2025, hivyo wananchi wasisahau kukichagua Chama Cha Mapinduzi waendelee kula matunda ya maendeleo yanayoletwa na serikli.
Amesema CCM kina viongozi shupavu na mahiri wakiwemo wabunge na madiwani walioaminiwa na wananchi,hivyo miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa weledi na viwango ni kwa sababu ya umahiri huo na usimamiza wa fedha.
Naye Katumwa amesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,wananchi wajitoke kuboresha taarifa zao katika daftari la wapiga kura ifikapo Agosti 21 hadi 27,mwaka huu,pia ambao hawajindisha hasa vijana wafanye hivyo ili wapate sifa ya kuchagua viongozi wao.
“Mwaka huu hatutaki mchezo, kwa maendeleo aliyofanya Dk.Samia ni kumpa kura za heshima za kumshukuru pia mbunge (Kiswaga),ni mbunge wa vitendo anayefika hadi vijijini, hivi mtampata wapi mbunge wa aina hii,”amesema.
Ameeleza kuwa kazi ya maendeleo aliyoifanya Rais Samia ni kubwa katika nchi yetu,shukurani pekee anastahili ushindi wa heshima ashinde kwa kishindo na ndio tunaouhitaji kwa kazi kubwa aliyofanya pia kura kwa wagombea wa CCM.
Katumwa amewataka vijana waliofikisha umri wa miaka 18 wakajiandikishe Katika Daftrai la Kudumu la Wapiga kura, waliopoteza shahada zao na waliohama maeneo wakaboreshe taarifa zao.
Awali Diwani wa Kisesa (CCM),Joseph Kabadi amesema uongozi ni sawa na timu ya mpira,maendeleo ya Magu na Kata ya Kisesa yamesababishwa na mbunge,diwani na wenyeviti wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji na wanachokifanya sasa ni kuwafafanulia wananchi wanafahamu miradi ya maendeleo iliyotekelezwa.
“Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu,wenyeviti hawa wakirudi madarakani tutafanya makubwa zaidi,zahanati ya Kitumba,zinahitajika sh.milioni 20 za ununuzi wa vifaa tiba,ujenzi vya vyoo na kichomea taka ili ikamilike wananchi wapate huduma wakiwemo wajawazito,”amesema.