Na Mwandishi wetu;-
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo anazotoa katika Jimbo hilo ili kuboresha huduma kwa Wananchi.
Mhe. Sillo ametoa pongezi hizo Julai 24, 2024 katika Kijiji cha Mwikatsi Kata ya Mamire wakati akizungumza na mamia ya Wananchi ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili huku akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Babati na wataalam mbalimbali kutoka sekta ya elimu, afya, miundombinu na nishati ili kutoa ufafanuzi na majibu ya hoja mbalimbali za Wananchi.
Amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi milioni 600 kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuwawezesha Wananchi wa Kata ya Mamire kupata huduma kwenye sekta zote.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumekuwa na utitiri wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Jimbo hilo huku akitaja baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa magumu kufikika lakini kwa sasa huduma za kijamii zimeendelea kusogezwa kwa kasi.
Aidha ameahidi kupeleka cherehani tatu kwa kikundi cha watu wenye uhitaji maalum katika Kijiji cha Mwikatsi ambapo awali alikikabidhi kikundi hicho cherehani mbili hivyo kufanya jumla ya cherehani tano.
Kwa nyakati tofauti Wananchi wa Kijiji cha Mwikatsi Kata ya Mamire Wilaya ya Babati wamemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, miundombinu na nishati.
“Mhe. Mbunge tunaomba utupelekee shukurani zetu za dhati kwa Mhe. Rais kuwa sisi Wananchi wa Kijiji cha Mwikatsi Kata ya Mamire tunamshukuru sana na tunamuuombea Dua kwa Mwenyezi Mungu na Afya njema”