Makamu Mkuu wa chuo cha mipango ya maendeleo vijijini upande wa taaluma Prof. Provident J.Dimoso akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea maonesho ya tano ya wiki ya elimu ya juu yanayoendelea huko Maisara Mjini Unguja.
Afisa Udahili wa chuo cha mipango ya maendeleo vijijini Rashid Mohamed Mandoa akijenga uelewa kwa vyombo habari juu ya huduma zinazopatikana chuoni hapo wakati wa maonesho ya tano ya wiki ya elimu ya juu yanayoendelea huko Maisara Mjini Unguja.PICHA NA FAUZIA
NA FAUZIA MUSSA
Vyuo Vikuu nchini vimeshauriwa kuanzisha mafunzo ya kazi za mikono zenye ubunifu na ujasisriamali ili kuwasaidia vijana kukabiliana na soko la ajira.
Akizungumza katika maonesho ya tano ya wiki ya elimu ya juu yanayoendelea huko Maisara Mjini Unguja, Makamu mkuu wa Chuo cha Mipango ya maendeleo vijijini Prof. Provident Dimoso, alisema hatua hiyo itawasaidia vijana kuanza kujiajira kabla ya kuajiriwa.
Aidha aliziomba taasisi za Serikali na binafsi kupendekeza fani ( kozi) za vipaombele katika ofisi zao kuanzishwa na vyuo vikuu hivyo jambo ambalo litawafanya vijana kuenda sambamba na matakwa ya ajira.
Mbali na hayo aliwataka wahitimu wa elimu ya sekondari kuitumia wiki ya maonesho ili kupata uelewa wa upatikanaji wa fursa mbali mbali za elimu ndani na nje ya nchi .
alieleza kuwa maonesho ya elimu za juuu hufanyika ili kutoa fursa za wanafunzi waliomaliza elimu ya sekondari kujiunga na vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi pamoja na kuimarisha ushikiano baina ya Taasisi za elimu ya juu na kuhakikisha sekta ya elimu inaendelea kuimarika nchini.
Kwa upande wake afisa udahili Chuo cha Mipango ya maendeleo vijijini Rashid Mohamed Mandoa aliwaomba Vijana kujiunga na Chuo cha Mipango ya maendeleo vijijini na kusema kuwa dirisha la udahili limeshafunguliwa na usajili wa wanafunzi wepya unfanyika bila malipo.
Alisema chuo cha mipango kinatowa taaluma mbalimbali kwa kuzingatia nadharia, vitendo, tafiti na mafunzo ya amali yanayomsaidia muhitumu kutoka chuo hicho kuweza kujiajiri na kuajiriwa pamoja na kinaimarisha mitaala ili kukabiliana na mabadiliko sekta ya elimu .
Alisema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mafanikio mbali mbali yamepatikana ikiwa ni pamoja na kutoa wataalamu wa mipango ya ardhi na mipango miji kulikochangia kupatikana kwa maendeleo mijini na vijijini.
Mwanzoni alisema Chuo hicho ni cha Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Wizara ya Fedha ambacho kilianzishwa mwaka 1979 chini ya Sheria ya Bunge na 28 ya mwaka 1980 na kuwashauri Vijana kujiunga na Chuo hicho ili kupata fursa mbalimbali za taaluma zinazoendana na soko la ajira.
Baadhi ya wanafunzi waliosoma katika chuo hicho akiwemo Munira Shamhun na Ahlam Abubakar Mahfoudh waliwashauri wanafunzi wanaomaliza masomo ya sekondari kusomea fani ambazo zinaendana na soko la ajira ili kujiajiri na kuajirika.
“serikali haitakuwa na uwezo wa kutuajiri vijana wote badala yake tunatakiwa kuangalia njia mbadala ya kujiajiri ikiwemo kusoma vyuo vinavyotoa taaluma za kazi za mikono na ujasisriamali ili kupunguza vijana wasio na ajira nchini.” Walisema vijana hao
Hata hivyo walisema wamevutiwa kujiunga na chuo cha mipango ya maendeleo ya vijijini kutokana na ubora wa taaluma zinazotolewa sambamba na mazingira rafiki na wezeshi chuoni hapo.
Maonesho ya 5 ya elimu za juu yameanza tarehe 5 -hadi 21 julai ,mwaka 2024 huko viwanja vya maisara yakiwa na kauli mbiu” ujuzi , umahiri na ubunifu katika elimu ndio nyenzo ya maendeleeo ya Taifa”