Mjumbe wa Tume ya Mipango na Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Kitaalamu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Dkt.Asha Rose Migiro akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelekea kwenye uzinduzi wa Kongamano la kwanza la kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
Mkurugenzi wa Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Thobias Makoba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelekea kwenye uzinduzi wa Kongamano la kwanza la kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Uzinduzi wa Kongamano la kwanza la kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya maendeleo ya Taifa 2050 kufanyika Jijini Mwanza kwa lengo la kukusanya maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Uzinduzi huo utafanyika Jumamosi Julai 20,2024 kuanzia saa tatu asubuhi katika ukumbi wa kwa Tunza Arena uliopo Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Thobias Makoba amesema Kanda ya ziwa imechaguliwa kuwa sehemu ya kuanzia kwa makongamano hayo kutokana na historia yake muhimu na nafasi yake kubwa katika Maendeleo ya Taifa.
Makoba amesema Kongamano hilo linatarajia kuongeza uelewa wa umma na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuunda dira ya miaka 25 ijayo ya Tanzania kupitia mpango wa Dira 2050.
“Kongamano hili la Mwanza ni la kwanza kati ya makongamano manne yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais,Tume ya mipango ambapo Kongamano lingine litafanyika Arusha Julai 24, 2024 na mengine katika Kanda zingine.
Kwaupande wake Mjumbe wa Tume ya Mipango na Mwenyekiti wa Timu Kuu ya kitaalamu ya Dira ya Taifa 2050, Dkt.Asha Rose Migiro, amesema Dira ni chombo mahususi kinachotumika kutoa mwelekeo wa nchi hususani katika maendeleo.