Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akifungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi, jijini Dodoma leo tarehe 19 Julai, 2024.
Wadau kutoka sekta mbalimbali za Serikali na binafasi wakiwa katika kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi jijini Dodoma leo tarehe 19 Julai, 2024.
Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Deogratius Paul akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi jijini Dodoma leo tarehe 19 Julai, 2024
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akiwa katika picha ya pamoja na wadau mara baada ya kufungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi jijini Dodoma leo tarehe 19 Julai, 2024.
…………
NAIBU Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ametoa wito kwa wadau wa mazingira kuwekea mkazo suala la nishati safi ya kupikia katika Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema hapa nchini wanawake hutumia muda mwingi kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kufanya shughuli za kujiingizia kipato hivyo ni muhimu kupanga mipango ya kushirikisha nishati safi katika masuala ya kijinsia.
Bi. Mndeme amesema hayo amesema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi, jijini Dodoma leo tarehe 19 Julai, 2024.
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi sekta za kiuchumi ambazo wanawake, wanaume, watoto, wazee, vijana na makundi maalum hutegemea kwa maisha yao ya kila siku.
Bi. Mndeme amesema sababu mbalimbali zikiwemo majukumu yao kijinsia, utamaduni, umri, uchumi, mila na desturi huchangia makundi hayo ya jamii kuathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Hii ni hatua kubwa katika uwezeshaji wa masuala ya jinsia hapa nchini, kama mnavyofahamu, Tanzania ni Mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris. Makubaliano ya Paris yanazitaka Nchi Wanachama kuandaa Mpango Kazi wa utekelezaji wa Programu ya Lima kuhusu masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Itakumbukwa kuwa Mkataba huo ulianzishwa mwaka 2014 katika mkutano wa 20 wa Nchi Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP20) uliofanyika Lima nchini Peru. Madhumuni ya LWPG ni kuzihimiza nchi Wanachama wa Mkataba kuhuisha masuala ya jinsia katika mipango kazi ya kitaifa ili kutekeleza Mkataba na Makubaliano ya Paris. Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais kama Ofisi Kiungo wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini, inaratibu maandalizi ya Mpango Kazi husika.
Hata hivyo, Bi. Mndeme amesema tafiti zimeonesha nchi zinazoendelea bado hazijahuisha Programu ya Lima katika mipango, sera na mikakati ili kuwezesha kuwa na takwimu za makundi hayo, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake katika majadiliano ya kimataifa, uhuishaji wa masuala ya jinsia katika sera, mipango na mikakati ya Taifa na kujenga uwezo wa kifedha, utaalam, fedha na taasisi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali tayari imehuisha masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi katika Sera ya Taifa ya Mazingira (2021), Mpango Kabambe wa Mazingira (2022-2032), Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026). Hivyo, maandalizi ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi ni mwendelezo ya Jitihada za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabainchi kwa kwa makundi yote ya kijamii ili kuweza kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.