Afisa Wanyapori wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Dunia Almasi,akitoa elimu ya kuzuia wanyama wakali na waharibifu hususani Tembo wanaotoka hifadhi na kwenda kwenye mashamba ya watu.
Afisa Mahusiano na Uhusiano wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere(TANAPA) kanda ya kusini kituo cha Kululu Stephen Mpondo akitwanga pilipili ambazo zinatumika kutengeza uzio wa kuzuia Tembo pindi wanapovamia mashamba ya wananchi.
Afisa Wanyapori wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Dunia Almasi kushoto,akiwaonyesha wakazi wa kijiji cha Changarawe kata ya Matemanga namna ya kutengeneza uzio wa pilipili unaotumika kuzuia wanyama waharibifu wasiingie kwenye mashamba.
Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Changarawe kata ya Matemanga,wakiangalia namna ya ufungaji wa uzio wa pilipili unaotumika kuzuia Tembo wasiingie kwenye mashamba na kula mazao.
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
KIKOSI cha askari kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kanda ya kusini kituo cha Kalulu,kimeweka kambi maalum katika kijiji cha Milonde wilayani Tunduru ili kusaidia kufukuza wanyama wakali na waharibifu hususani Tembo wanaotoka kwenye hifadhi na kuvamia makazi ya watu.
Askari hao watahusika kufukuza Tembo katika vijiji vya Changarawe,Namwinyu,Kajima,Kalulu,Milonde na Matemanga ambavyo vimekuwa na matukio ya wananchi kuvamiwa na Tembo mara kwa mara wakiwa katika shughuli zao.
Afisa Uhusiano wa Tanapa kituo cha Kalulu mkoani Ruvuma Stephen Mpondo alisema,kazi kubwa itakayofanywa na askari hao ni kuzuia Tembo kabla hawajafika kwenye mashamba ya wananchi na kuwarudisha kwenye maeneo yao.
Alisema,askari wataendelea kuwepo katika kijiji hicho kwa muda mrefu ili kuhakikisha wananchi wanabaki salama na wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali hasa kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo.
Amewataka wananchi na viongozi wa vijiji hivyo,kuhakikisha wanatoa taarifa haraka mara tu wanyama wanapovamia kwenye mashamba yao kabla hawajafanya uharibifu wa kula mazao.
Mpondo amewaomba wananchi,kuwapa ushirikiano askari ili waweze kutekeleza majukumu yao hasa ikizingatia kufukuza Tembo au wanyama wengine hatari siyo jambo rahisi na jepesi kunahitaji watu wenye uthubutu na waliopata mafunzo ya namna ya kukabiliana na wanyama hao.
Afisa wanyamapori wa wilaya ya Tunduru Dunia Almasi alisema,kwa muda mrefu Tembo wamekuwa wasumbufu kwa kuvamia mashamba na kufanya uharibifu wa kula mazao,kujeruhi na hata kuuwa.
Kwa mujibu wa Almasi,licha ya serikali kupitia Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kupeleka askari,wanaendelea kutoa elimu ya kuzuia na kufukuza wanyama hao kwa kutumia uzio wa pilipili,matofali ya pilipili na mabomu baridi.
Alisema,kutumia uzio wa pilipili ni njia sahihi kwani baadhi ya vijiji ambavyo wananchi wamepatiwa mafunzo na elimu hiyo matukio ya Tembo kuvamia mashamba na makazi ya binadamu yamepungua kwa kiwango kikubwa.
Amewataka wananchi wa Tarafa ya Matemanga na maeneo mengine wilayani humo,kuacha kulima kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi ili kuepuka kutokea madhara makubwa ya kuvamiwa na wanyama hao pindi wanapokuwa kwenye shughuli.
Badala yake amewashauri,kutafuta maeneo maalum kwa ajili ya kilimo cha pamoja hasa kwa mazao ya chakula na kuwezeshwa mbinu ili kuepuka uvamizi wa Tembo ambao wanarudisha nyuma jitihada za wananchi kujiletea maendeleo kupitia shughuli zao za kilimo.
“wakati umefika kwa vijiji kuanza kujipanga kwa kutafuta maeneo maalum kwa ajili ya kufanya shughuli zetu za kilimo,haiwezani mtu unakwenda kulima katikati ya msitu na wanyama hatari wakakuacha salama”alisema Dunia.
Ameeleza kuwa,mfumo wa maisha wa binadamu kwa sasa umebadilika kwa hiyo ni muhimu wananchi wakalim pamoja ili waweze kusaidiwa mbinu za kukabiliana na wanyama hao.
Diwani wa kata ya Matemanga Hamisi Kahesa,ameishukuru serikali kwa kuwapa mbinu mbalimbali za kukabiliana na Tembo kwani zimesaidia kupungua kwa matukio ya wanyama wakali na waharibifu kuvamia mashamba na kula mazao yao.