Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza leo na watumishi na wananchi wa Kijiji cha Mlimo, Kata ya Lufu iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi.
Sehemu ya watumishi na wananchi wa Kijiji cha Mlimo, Tarafa ya Kibakwe iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, wakati wa ziara yake ya kikazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mlimo mara baada ya kuwasili, ikiwa ni ziara yake ya kikazi
Baadhi ya Madiwani wa Viti maalum wakiimba mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kabla ya kumkaribishwa kwa ajili ya kuzungumza na watumishi na wafanyakazi katika eneo hilo
Diwani wa Kata ya Lufu Mhe. Gilbert Msigala akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlimo Kata ya Lufu iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Richard Maponda akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlimo, Kata ya Lufu iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene.
Na Lusungu Helela – Kibakwe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amepiga marufuku Watumishi wa Umma kusumbuliwa kufuatilia taarifa zao za kiutumishi wanapohamia kwenye kituo kipya cha kazi badala yake wafanye kazi zao kwani hilo sio jukumu lao bali ni wajibu wa Waajiri.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mlimo katika Kata ya Lufu, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma ambapo amesema suala la taarifa za Mtumishi ni jukumu la Mwajiri.
Amesema kitendo cha taarifa za watumishi kutohamishwa kumesababisha Watumishi hao kushindwa kupimwa kwenye mfumo wa e-tendaji kazi kwa vile kunakuwa hakuna taarifa za watumishi hao katika kituo kipya cha kazi na hivyo mwisho wake watumishi kusumbuliwa kufuatilia taarifa za kule walikotoka.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu- UTUMISHI kushirikiana na Mamlaka zingine zilikokasimiwa madaraka hayo ya kuhamisha Watumishi kuhakikisha Mtumishi pindi anapohama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine asisumbuliwe kuhusu taarifa hizo.
Hivyo Mhe. Simbachawene ametoa muda wa kuhamisha taarifa za watumishi waliohama kuwa ifikapo Agosti 15 mwaka huu taarifa za watumishi wote ziwe zimehamishwa na baada ya hapo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa wote watakaoshindwa kutekeleza jukumu hilo.
Amesema suala la kuhamisha taarifa za Mtumishi kutoka alikokuwa na kwenda kituo kipya cha kazi ni jukumu la Mkurugenzi au anayeongoza Taasisi wakishirikiana na Maafisa utumishi na kuongeza kuwa wanatakiwa kuhakikisha taarifa hizo zinahamishwa ndani ya mwezi mmoja ili watumishi waliohamishwa waendelee kufanya kazi zao kwa ufasaha.
“Utapimaje utendaji kazi wa mtumishi au kumpatia ruhusa mtumishi aliyepata dharula ilhali taarifa zake zipo sehemu nyingine, hii sio sawa, huko ni kuwatesa watumishi “amehoji Mhe. Simbachawene.
Amesema malalamiko ya kutohamishwa kwa taarifa za watumishi yamekuwa mengi kutoka kwa watumishi huku akiwataka watumishi wanapohama kutekeleza majukumu yao na hakuna atakayesumbuliwa.