Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf
………………
Ubalozi wa Tanzania nchini Oman umeandaa Kongamano
la biashara na uwekezaji litakalofanyika nchini Oman kuanzia tarehe 26 – 28
Septemba 2024.
Hayo yameelezwa wakati wa
kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa
Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf kilichofanyika
Julai 15, 2024.
Katika mazungumzo hayo, wawili hao walisisitiza
umuhimu wa kuanzisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Ushirikiano wa
nchi za Ghuba (GCC) na Jumuiya za kikanda ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Balozi Fatma alisisitiza pia umuhimu wa Oman
kushiriki maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam, maarufu Sabasaba
yanayofanyika kila mwaka mwezi Julai.
Kwa upande wake, Waziri Qais aliafiki mapendekezo
ya Oman kushiriki maonesho ya sabasaba ambapo aliahidi kuwa atatembelea
Tanzania na wafanyabiashara wakubwa ili kujionea fursa za uwekezaji
zinazopatikana nchini.
Alitoa mwaliko kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuzuru
Oman kwa lengo la kujionea maendeleo ya viwanda, hasa eneo la viwanda la Sohar
na kujadili namna ya kuanzisha makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara (MoU) baina
ya pande mbili. Alipendekeza ziara hiyo kufanyika katikati ya mwezi wa Septemba
au Oktoba 2024.
Viongozi hao walihimiza umuhimu wa usafiri wa moja kwa
moja wa ndege ya mizigo kati ya Tanzania na Oman ili kurahisisha biashara. Kufuatia
umuhimu huo, Balozi Fatma alieleza kuhusu kusainiwa kwa Mkataba mpya wa Ushirikiano
wa Anga (BASA) baina ta Tanzania na Oman Julai 16, 2024 utakaoiwezesha Ndege ya
Shirika la Ndege la Tanzania kufanya safari zake nchini Oman.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa viongozi hao kuhimiza
umuhimu wa kusaini Mkataba wa Kuepuka utozaji wa Kodi mara mbili ili kutimiza
azma ya kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili.
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf |
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf wakikabidhiana zawadi baada ya mazungumzo yao. |