Happy Lazaro,Arusha.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga kuboresha miundombinu ya Minada iliyopo nchini ili iweze kukidhi mahitaji ya watumiaji hasa katika sehemu za uzio, vyoo, maji, taa pamoja na mifumo ya malipo.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof Daniel Mushi alipotembelea Mnada wa Kimataifa wa Pugu uliopo Wilaya ya Ilala Jijini Dar Es Salaam kwa lengo la kufuatilia utekelezaji maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega mwezi Disemba 2023.
Prof. Mushi alisema kuwa maagizo yaliyotolewa na Mhe. Waziri ni pamoja na uboreshwajwi wa miundombinu ya mnada hasa upande wa taa zili mnada ufanyike kwa muda wa masaa 24, kuweka mazingira masafi ya watu kujisitiri pamoja na kuhakikisha maduhuri ya Serikali yanakusanywa vizuri.
“Kwa asilimia zaidi ya 90 maagizo yaliyotolewa yametekelezwa kwani taa zimewekwa, choo kipya kimejengwa kwa kushirikiana na halmashauri, na maduhuri ya Serikali yameongezeka. Kwa takwimu zilizopo kabla ya Disemba 2023, tulikuwa tunakusanya milioni 100 kwa mwezi, baada ya kuunda timu mpya na kufanya usimamizi mapato hayajawahi kushuka chini ya milioni 200.”amesema .
“Mnada huu tuliweka malengo ya kukusanya bil 2.4 kwa mwaka, na hadi kufika Disemba 2023 zilikusanywa milioni 700. Baada ya maboresho na kubadilisha uongozi, zimekusanywa bil 1.3 hii ni mara mbili ya makusanyo ya awali, tunafurahi maelekezo tuliyoyatoa yamefanyiwa kazi, maboresho haya tutayafanya kwa minada yote hapa nchini na yatakuwa ni endelevu.”amesema Prof. Mushi.
Kuhusiana kulalamikiwa kwa kukosekana sehemu ya kulishia Mifugo Prof. Mushi alisema kuwa mnadani sio sehemu ya kulisha Mifugo, mnada ni sehemu ya mauziano, Mifugo inaletwa ili iuzwe kwa wanunuzi lakini ikitokea Mfugo haujauzwa kwa siku husika ni vyema kutafuta namna ya kuihudumia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mnada wa Kimataifa wa Pugu Noel Byamungu ameushukuru uongozi wa Wizara kutembelea mnada huo kwani yeye pamoja na wasaidizi wake kwa kipindi kifupi wametekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega kwa kiwango cha kuridhisha na ameahidi kuyafanyia kazi maagizo mengine yaliyotolewa.
“Sisi kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya, tumejipanga kuendelea kuutangaza mnada kwa kuanzisha nyama choma kila jumamosi ili watu wautambue na pia uweze kutangazika kimataifa zaidi.” amesema Byamungu.
Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara wengine kwenye Mdana wa Kimataifa wa Pugu John Luma amesema kuwa Mnada huo kipindi cha nyuma kulikuwa na maeneo ya malisho, lakini kutokana na watu kujenga nyumba kuzunguka mnada, maeneo ya malisho yamekuwa ya shida.
Sambamba na hilo Luma ameishauri Serikali kuendelea kuboresha mnada huo kwani unatambulika kimataifa na ni jicho la nchi vilevile kuna kituo kikubwa cha Treni ya Umeme, wageni wengi watakuwa wanaongezeka.