Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa
Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) umemalizika leo tarehe 12 Julai 2024 jijini
Lusaka, Zambia.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na
Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 08 na 09 Julai 2024
jijini hapa umejadili na kupitisha agenda mbalimbali zenye lengo la kukuza na
kuimarisha hali ya siasa, ulinzi na usalama katika Kanda ya SADC.
Katika hotuba yake ya kufunga mkutano
huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe
ameshukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kushiriki kikamilifu kuchangia hoja mbalimbali
zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo na hatimaye kufikia makubaliano ya
pamoja.
Amesema licha ya kuwepo changamoto
kadhaa za amani na usalama katika kanda bado ana imani kubwa na nchi wanachama
kutokana na kuwa na nia ya dhati ya kuzimaliza ili kuwa na kanda yenye amani na
utulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Pia amewashukuru wajumbe hao kwa ushirikiano
waliompatia katika kipindi chote cha uenyekiti wa kamati hiyo na kuwaomba
kumpatia ushirikiano huo na zaidi wenyekiti ajaye ambaye ni Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Januari Makamba.
Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama
ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kusimamia na kulinda amani na usalama
katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi
cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano
huu uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. January Makamba akiwa ameongozana na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob
Mkunda, Balozi wa Tanzania nchini
Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano
wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na
Usalama.
Mhe.Makamba akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya ujumbe wa Tanzania wajumbe kutoka DRC walioshiriki Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC |