Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Bernard Kibesse kitabu cha Mpango kazi wa Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2024/2025 wakati wa Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi, Kenya tarehe Julai 08 hadi 12, 2024
……….
Serikali ya Tanzania imeliomba Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuendelea kuungana na Tanzania kwenye Agenda ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo itasaidia kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amesema hayo wakati ashiriki Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) unaofanyika Julai 08 hadi 12, 2024 jijini Nairobi, Kenya.
Amesema agenda hiyo ni muhimu kuungwa mkono kwani ina manufaa makubwa kwa utunzaji wa mazingira kwani itachagiza kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo huchangia ukatajai wa miti.
Pamoja na hayo pia, Mndeme ametoa wito kwa shirika hilo kuunga mkono katika Biashara ya Kaboni na Uchumi wa Buluu, masuala ambayo yanaleta tija katika kuinua pato la wananchi na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia mkutano huo, alisema Tanzania kama nchi mwanachama itapata fursa ya kuelewa shughuli za UNEP kwa mwaka uliopita na kueleza vipaumbele vya nchi ili viweze kujumuishwa kwenye mipango ya UNEP kwa mwaka mwingine wa utekelezaji wa mpango – (2024 – 2025).
Halikadhalika, Bi. Mndeme ametoa shukrani kwa UNEP kuendelea kuisaidia Tanzania hususan kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi, bioanuwai na uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Berdard Kibesse ameishukuru UNEP kwa jitihada za kupambana na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, Balozi Mhe. Dkt. Kibesse aliahidi Tanzania kuendelea kuwa wa mstari wa mbele katika kupambana na uharifu wa mazingira unaoikabili dunia na kuleta athari kubwa.
Aidha, mkutano huo unafanyika kwa lengo la kupitia programu za UNEP kwa kipindi cha mwaka 2022- 2023 na kupitia mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2023 – 2024.
Pia, katika mkutano huo wajumbe wanapitia utekezaji wa kazi za shirika hilo hususan kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi, bioanuwai na uchafuzi wa mazingira pamoja na kufanya maandalizi ya mikutano ijayo ya Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA – 7).