Na Mwandishi-WyKS
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameipongeza Mahakama kwa utendaji wake na kwa namna wanavyoshikamana na kuonesha upendo katika masuala mbalimbali ya Kijamii ikiwemo misiba.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo Julai 7, 2024 Tarime mkoani Mara wakati aliposhiriki katika dua maalumu ya kumwombea marehemu Amina Nyanda Juma ambaye ni mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof Ibrahim Juma ambaye alizikwa Juni Mosi, 2024, mkoani humo.
“Niwapongeze sana Mahakama kwa namna mlivyoshiriki toka mlipopokea taarifa za msiba, katika kipindi cha mazishi na leo katika arobaini ya Mama yetu. Namwona Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Waheshimiwa Majaji wa Mahakama za Rufani na Mahakama Kuu, Mke wa Jaji Mstaafu Mama Chande, Watumishi mbalimbali wa Mahakama hakika mmeonesha mshikamano na upendo katika kufanikisha haya yote. Unapoona mshikamano huu ujue yupo mtu ambaye yupo nyuma ya mafanikio haya na anatuunganisha sote na huyu ni Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma hivyo hatuna budi kumfariji yeye na familia yake na kushiriki katika dua hii.” Alisema Sagini
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha salamu za shukrani kwa niaba ya Jaji Mkuu amesema kuwa neno pekee alilolisema ni asante kwa yale yote yaliyofanyika katika kipindi chote cha msiba na Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki na kudumisha umoja huo.
Kadhalika, Prof. Elisante ameelezea kuwa, Wananchi wa Tarime wanapaswa kujiona kuwa nao ni sehemu ya Mahakama na kujivunia mafanikio ya Mahakama na kwa sasa Mahakama inaendelea kufanya maboresho mengi na ni vyema wakayafahamu na wakanufaika wa matunda ya maboresho ya Mahakama ikiwemo kutumia mfumo wa kupata mrejesho na kupata huduma kuhusu masuala ya Mahakama kwa kupiga namba 0752500400 bila malipo.