Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuzindua Bidhaa mpya za Mvinyo ( Wine) kutoka Kiwanda Cha Alko Vintages
Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Bw. Archard kato akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya Uzinduzi wa Bidhaa mpya za Mvinyo ( Wine) kutoka Kiwanda Cha Alko Vintages
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema kwasasa soko la Mvinyo unaozalishwa Tanzania limekuwa hadi kufika nafasi ya pili kwa ukubwa Afrika baada ya Afrika Kusini hivyo watahakikisha kiwango cha uzalishaji kinaendelea kukidhi viwango vya kimataifa.
Prof. Mkumbo aliyasema jana Julai 7,2024 Jijini Dodoma kwenye Hafla ya Uzinduzi wa Bidhaa mpya za Mvinyo ( Wine) kutoka Kiwanda Cha Alko Vintages ambapo aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wawekezaji ili wakulima wanaozalisha zao hilo waendelee kupata soko la uhakika na kuongeza thamani mazao ya kilimo.
“Kwakweli hiki ambacho mwekezaji amefanya kinaenda sambamba na ajenda ya Serikali ya uchumi katika suala zima la kuongeza thamani mazao ya kilimo nayeye anatusaidia kuongeza thamani kwenye zao hili la zabibu lakini sambamba na ajenda ya kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi”,alisema.
Alisema kwasasa Mvinyo wa Tanzania unakidhi sana viwango vya kimataifa kutokana na aina tofauti za uzalishaji zinazozalishwa pamoja na wanywaji kuongezeka.
Aidha, alitoa wito kwa wawekezaji kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na kuwapa sapoti wakulima ili waongeze uzalishaji.
“Kwasababu mwisho wa siku unahitaji malighafi ili uweze kuzalisha na malighafi hizi zinapatikana shambani, kwahiyo sisi setunatoa mbegu bora, tunaongeza masuala ya matumizi ya mbole na kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wetu waweze kulima wapate tija kubwa zaidi katika uzalishaji,”aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Bw. Archard kato amesema mabadiliko ya hali hewa yameathiri upatikanaji wa zabibu hivyo kwa mwaka huu hawategemei kupata malighafi nyingi ikilinganishwa na mwaka uliopita hivyo wataenda kuwasaidia wakulima ili wasiathirike tena na ukame.
“Ili tusiweze kuathirika na hii hali ya hewa hasa suala la mvua kuwa nyingi au wakati mwingine kuwa kidogo ndiyo maana tunataka kuingiza suala la kuweza kusaidia suala la visima ili tatizo la ukame lisiendelee kuwa kikwazo kwa wakulima wetu wa zabibu”, alisema.
Aliongeza kuwa kwasasa wataanza kutoa elimu kwa wakulima wa zabibu ili waweze kuhakikisha wanalinda mashamba yao dhidi ya magonjwa na hata magonjwa yakitokea waweze kuyamudu kwa kuwapatia na mikopo ili waweze kukabiliana nayo kwa kununua kadawa.