Wanawake wenye ulemavu uwe wa viungo, wasioona, viziwi, walemavu wa akili na aina nyingine za ulemavu wana haki na wanaweza kushiriki  katika michezo mbalimbali kama vile Mpira wa miguu (Amputee Football),  kuogelea, kukimbia, kurusha Tufe, Mishale, mbio za Baskeli za Maringi matatu (3) na michezo mengine kama walivyo wanawake wengine.

Tafiti zinaonesha kuwa njia pekee ya kuimarisha ustawi kwa jamii ya watu wenye ulemavu ni Elimu na Michezo, kwa upande wa elimu usawa wa kijisnia unazingatiwa  vyema lakini upande wa  michezo  wanaume wenye hali hiyo wanaonekana zaidi viwanjani ikilinganishwa na wanawake.

Taasisi za serikali na wadau wa michezo wanahamasisha michezo kwa wote ikiwa ni moja ya njia ya kujenga afya ,kupata ajira na  kuimarisha Uchumi kwa jamii hasa ya watu wenye ulemavu.

Baadhi ya jamii na familia  za watu hao  wanachukulia jambo hilo kuwa ni jambo lisilokubalika na kuwekezana jambo ambalo linarudisha nyuma na kupunguza idadi ya wanamichezo wanawake wenye ulemavu.

Makala hii inaangazia sababu mbalimbali zinazopelekea Wanawake wenye ulemavu kushindwa kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali Visiwani  Zanzibar.

BAADHI YA  WANAWAKE WENYE ULEMAVU WALIOJITOA KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO.

Bi Zawadi Khamisi, Mkaazi wa Darajabovu, mwenye  mwenye umri wa miaka 28 ni mke na mama wa watoto watatu,  amejiunga na chama cha  mpira wa miguu (Amputee Football) bila kujali hali yake ya  ulemavu na chanagamoto anazokabiliana nazo

Kwa sasa mama huyo hachezi mchezo huo ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchache wa wanamichezo wanawake wenye ulemavu,lakini anaenda viwanjani na kufanya mazoezi kila chama hicho kinapohiaji.

Bi Zawadi  alisema wanawake wengi wenye hali hiyo hawana mwamko wa kushiriki katika michezo ikiwemo amputee football kutokana na kutokuwepo na miundombinu rafiki ya Viwanja vya kufanyia mazoezi, pamoja na  kukosa fedha kwa ajili ya nauli na kutafutia vifaa vya michezo.

“Tunaishi mbali na viwanja vya kufanyia mazoezi na wiki nzima tunatakiwa kuhudhuria mazoezi, baadhi yetu hatuna hata kazi za kutuingizia kipato nauli hiyo tutaitowa wapi na hali hizi tulizonazo? , kama hutukuwezeshwa wanawake wenye ulemavu  kwa kweli hatuwezi kushiriki katika michezo.”alieleza Bi Zawadi.

Ameeleza kuwa kutokana na hali walizonazo wanahitaji usafiri angalau wa Bajaji ili kuweza kufika viwanjani kwa wakati na bila kuchoka kwani masafa yaliopo baina ya vituo vya Daladala hadi kufika eneo hilo  ni mbali kulingana na hali zao.

“Mimi nina mguu mmoja, nashushwa tobo la pili, hata nikifika Maisara au Mnazimmoja nimechoka na mara nyengine kuchelewa na kushindwa kufanya mazoezi, mfano hai umeuona hapa,sisi tunatakiwa tufike saa 8 za mchana unaona hadi sasa hivi saa 10 hii watu hawajafika,tukiwa na usafiri wa uhakiki itasaidia kuongeza ushiriki wetu.”aliesema mama huyo.

Hivyo aliishauri Serikali kutambua uwepo wao na kubuni mbinu rafiki zitakazowasaidia watu hao wakati wanapotumia usafiri wa umma .

“hata kutotozwa nauli wakati tunapopanda daladala na kutushusha sehemu rafiki, itakuwa msaada mkubwa kwetu na kutasaidia kuongeza idadi ya ushiriki wetu, kwani baadhi ya gharama itakuwa zimetupungukia” aliomba Bi Zawadi.

Pia aliwashauri wanawake wengine wenye ulemavu kujitokeza kuungana  nao ili  kuweza kupata timu ya wanawake wenye ulemavu wa mpira wa miguu na waweze kupata fursa kupitia mchezo huo.

Bi Amina Daudi  Simba ni mwanamichezo kwenye chama cha michezo ya watu wenye ulemavu wa viungo anaeshiriki michezo tofauti kama kuogelea, basketball wall chair, kurusha mishale pamoja na mbio za Baskeli ya maringi matatu ndani na nje ya Tanzania amesema mitazamo hasi kwa baadhi ya familia za watu hao ni kikwazo cha kushiriki katika michezo.

“Baadhi ya familia za  watu wenye ulemavu  haziwaungi mkono watu hao kushiriki katika  michezo wakiamini kufanya hivyo ni sehemu ya kumdhalilisha msichana na mwanamke mwenye ulemavu” alisema mwanamichezo  huyo.

Bi Amina, anaeishi na dada yake maeneo ya Fuoni nyumba moja amesema familia yake sio kikwazo cha yeye kushiriki michezo kama ilivyo kwa familia za wanawake wengine wenye ulemavu.

Bi Amina   aliwashauri wazazi na walezi kutokuwaficha wanawake na wasichana wenye ulemavu na badala yake kuwatoa katika maeneo mbalimbaliya jamii ikiwemo viwanjani ili kujenga hamasa ya wao kushiriki katika michezo kama wanavyoshiriki wengine ili kuongeza idadi ya  wanamichezo wanawake wakiwemo wenye ulemavu.

“Jambo lolote ni lazima ulipende na liwe ndani ya damu yako, ikiwa michezo haipo katika damu yako kamwe hutoweza kushiriki kwani changamoto ni nyingi sana hasa kwetu sisi wenye ulemavu.”  Alimalizia Bi Amina

KAULI YA VYAMA VYA MICHEZO JUU YA USHIRIKI WA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KATIKA MICHEZO.

Mjumbe wa kamati ya michezo kwa watu wenye ulemavu wa viungo Ali Abdalla Khatibu  amesema kadiri siku zinavyokwenda mbele ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo unapungua kutokana na  jamii kutokuwaamini na kuwakatisha tamaa.

Bwana Ali aliwaomba wadau wamichezo kuendelea kutoa elimu ili kuondoa mitazamo hasi ya jamii juu ya ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo ili kuongeza idadi ya ushiriki wao na kuweza kujipatia maendeleo kupitia sekta ya michezo.

Hata hivyo aliwaomba wadau wa michezo kuwashirikisha watu wenye uleamvu katika mabonaza mnbalimbali yanapofanyika ili kuongeza hamasa za wengine kujitoa na kushiriki katika michezo kwa maendeleo.

Bi Saada  Hamadi Ali ni mwenyekiti wa chama cha michezo cha watu wenye ulamavu wa akili Zanzibar  na mzazi wa watoto wenye ulemavu amesema ushiriki wa wanawawake wa kundi hilo bado upo chini kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha katika vyama vya michezo vya watu hao  kuweza kuwasaidia kujitokeza viwanjani kwa wingi.

 “vyama vyetu vinaendelea  kuhimiza  familia za watu hao kuwaleta katika  michezo lakini bado baadhi ya familia hazipo tayari kujitolea,wanachotaka  ni kuona  chama kiwawezesha kwa kila kitu jambo ambalo ni gumu kutokana na uwezo mdogo wa kifedha tulionao.”

Ameeleza kuwa familia nyingi zinapopata mtu mwenye ulemavu huchukulia kama sehemu ya mkosi na kuamua kuwaacha  nyuma katika mambo mbali mbali  ikiwemo masuala yakushiriki katika  michezo, hali hiyo inachangia wanawake na wasichana wenye ulemavu kushindwa kushiriki michezo hiyo.

Ameongeza kuwa  ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo ni mdogo ukilinganisha na wanawake wasio na ulemavu kutokana na mitazamo ya baadhi ya jamii kuwa kumshirikisha mwanamke mwenye ulemavu  na hata asie na ulemavu ni  sehemu ya uhuni.

Bisada ambae pia ni Mjumbe wa  Kamati ya Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu JUWAUZA alitoa rai kwa serikali, wahisani wafadhili na wadau wa michezo kuviwezesha  vyama vya michezo vya watu wenye ulemavu ili kuongeza idadi ya ushiriki wao viwanjani.

WADAU WANAVYOWAUNGA MKONO WANAWAKE WENYE ULEMAVU KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO

Tamko la sera ya michezo ni kuwa Serikali itahaskikisha watu wenye mahitaji maalum wanapatiwa fursa sawa za kushiriki katika michezo pamoja na kuweka mikakati ya kushajihisha watu kutowaficha watu hao na badala yake kuwashajihisha kushiriki katika  michezo.

Mikakati  ya sera hiyo ni pamoja na kuandaa utaratibu wa kuwapatia mafunzo watu hao,kuandaa program za uinuaji wa vipaji vyao kuanzia Shehia,Wilaya ,Mkoa hadi Taifa ili kujiendeleza kimichezo,kuandaa utaratibu wa kuwapatia tunzo wanaofanya vizuri pamoja na kuzisaidia timu za watu wenye ulemavu kushiriki katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar ZFF  Sleiman Mohammed Jabir amesema shirikisho hilo linatambua haki za watu wenye ulemavu kikatiba pamoja na kusaidia  mahitaji yao pale yanapohitajika ili kurahisisha shughuli zao za kimichezo zinazopelekea kuwajenga  kimwili na kiakili sambamba na kujipatia fursa mbalimbali za kimichezo.

“Hivi karibuni kulikua na timu ya wasichana iliyoanzishwa na taasisi ya WEZA lakini kama sisi  ZFF ambao ni walezi wa wachezaji wa mpira wa miguu tuliishauri  timu hiyo kuhakiksha wanawashirikisha wanawake wenye ulemavu kwenda kuiwakilisha Zanzibar nje ya nchi  ambapo mchezaji mmoja mwenye ulemavu wa ngozi alikwenda nchini ufaransa kushiriki mashindano kupitia weza na zff,hizo ni miongoni mwa jitahada zetu” alisimulia Rais wa ZFF

Bwana Sleiman amesema licha  ya juhudi hizo  lakini bado ushriki wa wanawake wenye ulemavu ni mdogo kutokana na  baadhi yao kutokujikubali na kujiskia aibu kutokana na hali zao.

Hali hiyo hururudisha nyuma  jitihada za baadhi ya wanawake wenye ulemavu  walioamua kushiriki katika  mchezo na hata kuwakatisha tamaa na  kushindwa kufikia malengo.

 “hadi sasa hakuna timu ya mpira wa miguu ya wanawake wenye ulemavu wa viungo kutokana na uchache wa watu hao viwanjani, sheria za mpira huu ni lazima timu iwe na wachezaji 12 na  waliojitokeza ni kidogo .”alibainisha rais huyo.

 Rais wa ZFF ameitaka jamii kubadilika na kuwatoa wanawake wenye ulemavu  kuweza kuonesha uwezo wao katika michezo na kuweza kunufaika .

Katiba ya shirikisho la mpira wa miguu ZFF ya mwaka 2018 toleo la 2021 inaonesha kuwa miongoni mwa wanachama wa shirikisho hilo ni watu wenye ulemavu wa viungo bila kujali jinsia.