Na Mwandishi wetu,Masasi
MATUKIO ya watu kujeruhiwa na kuuwa na wanyama wakali kama Simba,fisi na viboko katika kijiji cha Lichehe kata ya Sindano wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, pindi wanapokwenda kuchota maji katika mto Ruvuma yamemalizika.
Ni baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira(Ruwasa),kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Lichehe-Mgwagule ulioleta faraja kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho baada ya kuanza kupata huduma ya maji safi na salama kwenye makazi yao.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Masasi Simon Fute alisema,mradi wa maji Lichehe Mgwagule umejengwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa gharama ya Sh.185,000,000 kwa sasa umekamilika kwa asilimia mia moja na unatoa huduma ya maji kwa wananchi.
Alisema,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu kinachotosheleza mahitaji ya maji kwa wananchi wa kijiji cha Lichehe,ambao kwa muda mrefu hawakuwa na huduma ya maji ya uhakika badala yake walitegemea visima vya asili na maji ya mto Ruvuma.
Alisema,kutokana na changamoto hiyo,serikali iliamua kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji ili kuwaondolea kero ya huduma ya maji safi na salama wananchi wa kijiji hicho ambao tangu Uhuru hawajawahi kushuhudia maji ya bomba katika kijiji chao.
Kwa mujibu wa Fute, kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 100,000,kujenga vituo vya kuchotea maji vinne,kuchimba kisima,kujenga nyumba ya mashine na mtandao wa mabomba umbali wa kilometa tatu.
Fute,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,waziri wa maji Jumaa Aweso na Mtendaji Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo kwa kuleta fedha zilizofanikisha kutekeleza mradi huo na viongozi wa kijiji hicho kwa ushirikiano waliotoa wakati wa utekelezaji wa mradi.
Kwa upande wake Mhasibu wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO Lulindi) Amina Hassan alisema,kwa sasa wanahudumia vijiji 51 vyenye wateja zaidi ya 1,739 kati yao watu binafsi ni 1,500 wanapata huduma kwa kuunganishiwa maji majumbani na wengine wanachota maji kupitia vituo maalum(DPS).
Alisema tangu wapoanza kutoa huduma ya maji,wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Milioni 18 zilizotokana na mauzo ya maji,hata hivyo changamoto kubwa katika uendeshaji wa mradi huo ni taasisi za serikali kutolipa ankara za maji kwa wakati.
“fedha tunazodai kutoka kwa taasisi za serikali ni zaidi ya Sh.milioni 20,tunaziomba taasisi zinazodaiwa kulipa madeni yao kwa wakati ili tuweze kutoa huduma bora kwa wananchi,madeni haya yanatukwamisha sana katika uendeshaji wa mradi huu” alisema.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lichehe Issa Nyika alisema,kukamilika kwa mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Lichehe kwa kuwa umemaliza kero ya huduma ya maji, hofu na mateso ya kushambuliwa na wanyama wakali na kila wanapokwenda kuchota maji kwenye visima vya asili na mto Ruvuma.
Aidha alisema,mradi wa maji Lichehe-Mgwagule umesaidia wananchi kupata muda mwingi wa kushiriki katika shughuli za maendeleo,tofauti na hapo awali ambapo walilazimika kuamka usiku wa manane kwenda kuchota maji kwenye bonde la Mgwagule na wengine katika Mto Mmwiti umbali wa kilometa 5.
“kabla ya mradi huu wananchi hasa akina mama walipata mateso makubwa ya kuamka saa tisa usiku kwenda kufuata maji katika kitongoji cha Mgwagule kilichopo umbali wa kilometa 5 ambako kuna kisima cha asili,karibu wananchi wote wa Lichehe walitegemea kupata maji hapo na wakitoka saa mbili asubuhi wanarudi saa tisa jioni”alisema.
Pia alisema,baadhi ya wananchi walikwenda hadi mto Ruvuma ili kuchota maji baridi (yasiokuwa na chumvi),lakini changamoto kubwa ilikuwa wanyama wakali wakiwemo Simba,Tembo,Viboko na Fisi waliotishia maisha yao.
Mkazi wa kijiji la Lichehe Hussen Ibrahim,ameishukuru serikali kwa kuwaondolea adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ambayo ilikwamisha ushiriki wao wa kazi mbalimbali za kujiletea maendeleo.
“tunaishukuru sana serikali ya mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan,hata hivyo tunaiomba itafute chanzo kingine ambacho kina maji baridi kwani tunayotumia kwa sasa yana asili ya chumvi”alisema Hussen.
Fatma Yasin alisema,baadhi ya wanawake na watoto wa kijiji hicho wamepoteza maisha kwa kuuawa na wanyama wakali na wengine kupata ulemavu wa kudumu baada ya kushambuliwa na wanyama hao walipokwenda mto Ruvuma kuchota maji.