Makamu wa kwanza wa Rais Mhe.Othman Masoud Othman akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni mbili na laki tano kwa aliekua Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt Omar Dadi Shajak, wakati wa hafla ya kagwa kwake kwa kumaliza utumishi wa umma huko Ukumbi wa golden tulip Uwanja wa ndege Zanzibar .
Na Fauzia Mussa.
Makamu wa kwanza wa Rais Mhe. Othman Massoud Othman ametaka kuzingatiwa utaratibu wa kuwapata watumishi wenye vipaji, uwezo, na wenye kufuata misingi ya uadilifu ili kusimamia vyema maendeleo na maslahi ya umma.
Mhe. Othman ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumuaga aliekua Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt. Omar Dadi Shajak huko Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema ili nchi ifikie maendeleo ya kweli, ni wajibu kwa viongozi wa umma kuzingatia misingi ya sera, uadilifu, na moyo wa kujitoa katika utumishi, na kuachana na kufanya kazi kwa maslahi binafsi jambo ambalo linadhoofisha kasi ya maendeleo katika jamii.
Mhe.Othman amemtaja dkt.Shajak kuwa alikua kiongozi bora na wakupigiwa mfano hadi kufikia kuagwa Kwa kukamilisha Utumishi uliotukuka.
Hivyo amewataka viongozi na wafanyakazi wanaoendelea kutumikia umma kufuata nyayo za mstaafu huyo ili wawe na mwisho mwema katika maisha yao ya utumishi.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu mkuu kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said amewataka watumishi wa umma kuiga mfano wa Dkt Shajak kutokana na utendaji na uongozi wake uliotukuka sambamba na kuacha alama nzuri katika sehemu mbalimbali alizowahi kuongoza.
“Dkt. Shajak ameongoza taasisi mbalimbali za Serikali ambapo sehemu zote hizo alionekana kufanya vizuri, kitendo cha kugawa kiongozi huyu kwa namna yake kunaonesha wazi mazuri aliyowacha wakati wa kutekeleza majuklumu yake.” Alisema Mhandisi Zena.
Amewasihi wafanyakazi na viongozi kuiga mfano wa Dkt. Shajak ili waweze kumaliza Utumishi wao kwa wema na kusimuliwa vizuri kwa watakakuja baada yao.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Sleiman amewataka Wafanyakazi na Viongozi wengine kuiga mfano Dkt. Shajak na kuwa hafla hiyo ni sehemu ya kujitathmini na kuwa somo kwa wafanyakazi na viongozi wengine ili kuweza kujua namna ya kuishi katika maisha ya Utumishi wa umma.
Amesema kuwa katika kipindi kifupi alichofanya kazi na kiongozi huyo amebaini kuwa Dk. Shajak ni kiongozi anaejali wafanyakazi wake hivyo amewataka kubadilika na kujifunza kupitia nyayo zake.
Akizungumza kwa njia ya simu Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Bw. Abdalla Hassan Mitawi amesema tukio hilo linaakisi kutambua mchango wa Dkt. Shajak kutokana na uongozi wake ulio mzuri.
Amesema Ofisi hiyo itamkumbuka kiongozi huyo kwa jitihada zake na mashirikiano aliyokua nayo katika Ofisi hiyo hasa katika masuala yaliyohusiana na mazingira.
Aakitoa salamu za Wafanyakazi wenzake, Mwanasheria wa Ofisi hiyo Saada Mussa Said amesema kiongozi huyo alitumia busara na hekima pamoja na kufanya maamuzi mazuri katika utendaji wake ili kuimarisha na kuwajenga watendaji wenzake.
Aidha Wafanyakazi hao wameahidi kuyatunza na kuyaendeleza yote aliyowaelekeza na kumkumbuka milele kutokana na alama alizoziacha kwa Wafanyakazi hao katika utendaji wao.
Hata hivyo wameomba kuwapokea wafanyakazi hao,wakati watakapohitaji msaada wake ili kuendelea kuchota hekima na busara zake kama walipokuwa pamoja katika utendaji wa kazi.
Mbali na hayo wamesema kustaafu kwake isiwe mwisho wa kukutana nao na kumuomba awapoke wakati wowote katika shughuli za kiserikali na kijamii.
Vile vile ametumia fursa hiyo, kumuomba Dkt. Shajak kuwasamehe kwa yale yote waliokosea wakati alipokuwa akiwaongoza.
Akitoa neno la shukrani baada ya kukamilika kwa tafrija hiyo aliekua Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt. Omar Dadi Shajak ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais kwa heshima waliompatia kutokana na Utumishi wake.
Dkt. Omar Dadi Shajak alianza kufanya kazi katika Utumishi wa umma mwaka 1991 na kustaafu mwaka 2024 Katika ofisi ya Makamu wa kwanza wa rais akiwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, na wa kiongozi huyo anaagwa kwa kumaliza utumishi uliotukuka, Kitabu cha Historia yake kilizinduliwa .
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Saada Mussa Said akitoa salamu za wafanyakazi wa Ofisi hiyo katika hafla ya kumuaga Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt.Omar Daji Shajak Kwa kumaliza muda wake wa utumishi wa umma huko Golden tulip uwanja wa ndege Zanzibar.
Baadhi ya Makatibu wakuu wa SMZ wakiwa katika hafla ya kumuaga Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt.Omar Dadi Shajak Kwa kumalizamuda wake katika Utumishi wa umma hafla iliyofanyika Ukumbi wa golden tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.
Makamu wa kwanza wa Rais Mhe.Othman Masoud Othman akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni mbili na laki tano kwa aliekua Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt Omar Dadi Shajak, wakati wa hafla ya kagwa kwake kwa kumaliza utumishi wa umma huko Ukumbi wa golden tulip Uwanja wa ndege Zanzibar .
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said (kushoto) akipokea kitabu cha simulizi fupi ya aliekua Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt Omar Dadi Shajak kutoka kwa waziri wa Nchi ofisi ya makamu wa kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman kilichozinduliwa katika hafla ya kumuaga kiongozi huyo iliyofanyika Ukumbi wa golden tulip Uwanja wa ndege Zanzibar .
Waziri Mstaafu Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Fatma Fereji pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya idara ya habari maelezo Zanzibar Yussuf Omar Chunda wakiwa katika hafla ya kumuaga Katibu Mkuu Ofisi hiyo huko Golden tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe.Othman Masoud Othman (kulia) akimkabidhi kitabu cha simulizi fupi ya aliekua Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt Omar Dadi Shajak,Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa pili wa Rais Mhe. Hamza Hassan Juma kilichozinduliwa katika hafla ya kumuaga kiongozi huyo baada ya kumaliza muda wake katika utumishi wa umma iliyofanyika Ukumbi wa golden tulip Uwanja wa ndege Zanzibar .
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR