Mgeni Rasmi, Prof. James Mdoe (wa tatu kushoto akiwa ameketi), Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la TEWW, Dkt. Naomi Katunzi (kulia kwake), Mkuu wa Taasisi, Prof. Michael Ng’umbi (kushoto kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa mahafali ya 62 yaliyofanyika Dar es Salaam tarehe 26 Juni 2024.
Baadhi ya wahitimu wakifurahi katika mahafali ya 62 ya kutunuku vyeti, stashahada na shahada za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika Jumatano, Juni 26, 2024, katika Kituo cha Kitaifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi, akiwahutubia wahitimu wakati wa mahafali ya 62 ya programu za cheti, stashahada, na shahada za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima tarehe 26 Juni 2024, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
………..
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia , Prof. James Mdoe ameipongeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kuandaa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima katika ngazi ya astashahada, stashahada na shahada.
Prof. Mdoe ametoa pongezi hizo wakati wa mahafali ya 62 yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Juni, 2024 akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda.
Prof. Mdoe amesema kuwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ambayo ni kuandaa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya na mnayoifanya lakini inabidi Taasisi hii kuongeza ubunifu kwa kutoa mafunzo ambayo yana uhitaji mkubwa katika soko la ajira, pamoja na kutoa mafunzo ambayo yanaenda sambamba na sayansi na teknolojia.” Alisema Prof. Mdoe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Prof. Michael Ng’umbi amesema jumla ya wahitimu 482 wamehitimu ambapo wanaume ni 154 sawa na 32% na wanawake 328 sawa na 68%. Wahitimu hao walipata mafunzo katika kampasi za Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza katika Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii pamoja na Elimu Masafa.