Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Sospeter Mtwale,akizungumza wakati akizindua Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,hafla iliyofanyika leo Juni 27,2024 jijini Dodoma.
KAIMU Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa Mhe.Anthony Mtaka ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,hafla iliyofanyika leo Juni 27,2024 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Mohamed Mchengerwa, akizindua Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,hafla iliyofanyika leo Juni 27,2024 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Mohamed Mchengerwa,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,hafla iliyofanyika leo Juni 27,2024 jijini Dodoma.
……
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Mohamed Mchengerwa ,amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wanaongeza kasi ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo inatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa gharama ya sh. bilioni 400 ambao utagharamiwa na serikali pamoja na washirika wa maendeleo.
Mhe. Mchengerwa amewataka watendaji hao kutomsubiri Rais Dk. Samia Suluhu Hassan afanye hivyo kwakuwa wamepewa mamlaka makubwa ya kusimamia maeneo yao.
Mhe. Mchengerwa amesema dhamira ya programu hiyo ni kuamsha chachu ya utendaji kazi katika maeneo yao ya utawala huku akieleza kuwa kazi kubwa imeshafanyika.
“Leo hii tukimsimamisha kila mkuu wa mkoa hapa ataeleza mabilioni yaliyoingia katika mkoa wake, hatuna sababu yoyote ya kurudi nyuma kwa kazi kubwa ambayo Dk. Samia amefanya.
Rais ametuletea programu hii ili tuboreshe maeneo ya utendaji kazi wetu, kazi tuliyobaki nayo ni utoaji wa huduma, kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.”
Aliongeza kuwa “Ninakiri kazi kubwa ambayo wakuu wa mikoa mnafanya, nilipoingia na sasa tofauti ni kubwa sana watendaji wanafanya kazi, umoja na mshikamano umeimarika.”
“Rais anawaona mnapoenda site na kusikiliza kero za wananchi anawaona, kazi tuliyonayo sasa ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, Rais amenituma niseme hii, sasa hivi watu hawakai maofisini kama ilivyokuwa zamani, ule U-mungu mtu umekwisha. tuendelee kujishusha kuwa wanyeyekevu kwa watanzania kwa sababu ndio wenye nchi yao.
Nchi hii ni ya wananchi hakuna namna , niliwaambia ukiwa mkuu wa mkoa au kiongozi ndani ya serikali ukijishusha cheo chako hakiwezi kuondoka kitabaki palepale, lakini tutaendelea kuongeza imani kwa wananchi wetu.”
Alisisitiza kuwa Rais anafurahishwa na utendaji wa wakuu wa mikoa huku akimtolea mfano Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda anafanya vizuri.
“Tunatambua yapo maeneo wasaidizi wetu bado hawajatuelewa vizuri tuna budi kuwasaidia ili waweze kutuelewa maana kuna wengine wanahisi masuala mengine sio yao mfano miradi hivyo hii lazima tukairekebishe.
Shusheni maelekezo kwa wakuu wa wilaya Mradi wowote unapoharibika kwenye eneo lako ni la kwako hata kama limefanywa na mtendaji mwingine hivyo tuongeze jitihada za kusikiliza kero na kuwahudumia wananchi ipasavyo.”
Alisema kila mkuu wa mkoa ana hulka ya utendaji kazi hata hivyo serikali inataka kuona kero zikitatuliwa moja kwa moja kwa wananchi kule chini na kwamba uwe utendaji wa ubunifu ili kupunguza malalamiko kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu programu hiyo, alisema uazishwaji wake ni mwendelezo wa juhudi za serikali kupanua wigo wa ugatuaji wa madaraka kwa wananchi kwa kuimarisha Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Alisema kupitia programu hizi mafanikio kadhaa yalipatikana ikiwemo kuimarika na kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika chaguzi za kisiasa katika ngazi za msingi na kuongezeka kwa ruzuku kutoka serikali kuu kwenda mamlaka za serikali za mitaa.
Aidha, kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na kuongezeka kwa mapato ya ndani, kuongezeka kwa ugatuaji wa rasilimali watu kwa mamlaka hizo, kuimarisha uwezo wa Ofisi ya Rais, Tamisemi na utoaji huduma kwa wananchi.