MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO Bw.Thobias Makoba,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 27,2024 jijini Dodoma kuhusu maazimio ya kikao baina ya Serikali na uongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara nchini.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKAL na uongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara nchini wameafikiana kumaliza mgomo wa wafanyabiashara kwa kuweka maazimio 15 ikiwemo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusitisha Mara moja mazoezi yote ya kamata kamata pamoja na kusitisha mazoezi mengine yote ya ufuatiliaji wa risisti za EFD katika maeneo yote nchini hadi ifikapo Agosti mwaka huu.
Akisoma maazimio hayo Leo Juni 27,2024 jijini Dodoma na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO Thobias Makoba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao baina ya Serikali na uongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara nchini.
Aidha imeelekezaTRA kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini kuanzia Julai, 2024.
Bw.Makoba ametaja maagizo mengine kuwa ni Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuongeza haraka Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation.
“TRA imeelekezwa kuongeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho ya kodi yanayofanyika ili kuwezesha kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi nchini. Aidha, Taasisi husika za serikali pamoja na mabaraza ya biashara yashirikishwe kikamilifu katika ngazi zote,”amesisitiza
Ameongeza kuwa :”TRA pia inaelekezwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika. Bidhaa hizo ni Vitenge, Mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti,”.
“Serikali imeelekeza Wizara ya Fedha kuratibu zoezi la kufanya uchambuzi, tathmin na mapitio ya mfumo mzima wa utozaji na ukusanyaji pamoja na viwango vya Ushuru wa Huduma pamoja na kushauri njia mbadala ya utozaji itakayo kuwa rafiki zaidi kwa wafanyabiashara ili kulinda mitaji na ukuaji wa biashara nchini.
Kuhusu wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na mamlaka zingine husika itaendelea kuimarisha ukaguzi wa vibali vya kazi kwa wageni ili kuhakikisha kuwa wamiliki wa vibali hivyo wanafuata masharti ya vibali hivyo kwa mujibu wa Sheria za nchi.
“Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka sheria, Kanuni, Taratibu na masharti ya vibali vya ajira ikiwa ni pamoja na kuwafukuza nchini na waajiri husika kuchukuliwa hatua za kisheria.
aliongeza kuwa :”Kutokana na maazimio haya na maagizo ya serikali, pande zote mbili zimekubakiana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa watanzania huduma wanazostahili.
Makoba alisisitiza kuwa :”Kwa maslahi mapana ya nchi yetu, serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wote kama ambavyo Mheshimiwa amekuwa akisisitiza katika uongozi wake,”.