Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Said Mtanda akizungumza katika Barazala Madiwani wa Manispaa ya Ilemela, lililoketi leo kujibu hoja za ukaguzi wa CAG.
NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela,mkoani Mwanza imeendelea kupata hati safi (unqualified opion),kwa miaka mitano mfululizo,kwa mujibu taarifa ya hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.
Mkaguzi wa Nje,Athuman Mustapha amesema leo alipowasilisha katika Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo taarifa ya CAG kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/23 hoja 17 za ukaguzi zimetekelezwa huku hoja saba zikiwa katika hatua za utekelezaji na kutaja sababu ya kutofutwa kwa hoja hizo ni kukosekana kwa baadhi ya vielelezo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa (local Government Finance Act 1982),iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019,kila baada ya mwaka wa fedha kwisha halmashauri zinapaswa kuwasilisha taarifa zake za hesabu kwa CAG kwa ukaguzi na baada ya ukaguzi huo halmashauri hupewa nafasi ya kujibu hoja.
Mkuu Wa Mkoa wa Mwanza (RC),Said Mtanda ambaye amehudhuria kikao hicho cha Baraza la Madiwani,mara baada ya taarifa hiyo ameipongeza Manispaa ya Ilemela kwa kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitano mfululizo.
Amesema kitendo cha manispaa hiyo kupata hati inayoridhisha kwa miaka mitano,kinaonesha jinsi gani msimamizi wa halmashauri ambaye ni mkuu wa mkoa amefanya kazi nzuri.
Mtanda amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo,Ummy Wayayu kuhakikisha hoja zilizobakia zinafutwa pia,awasilishe ofisini kwake (RC) Mkoa,mpango kazi wa kujibu hoja hizo kupitia Katibu Tawala (RAS) ifikapo Juni 28,maka huu.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameuagiza uongozi wa manispaa hiyo kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa CAG katika ukaguzi wa hesabu za mwaka 2023/2024 ili kushughulikia hoja hizo kwa wakati na kuwezesha zote kufutwa.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela,Renatus Mulunga kwa niaba ya madiwani amemshukuru Mtanda kwa maelekezo na kuahidi kuendelea kuwasimamia watendaji ili kuhakikisha hoja zilizobaki zinajibiwa kwa wakati.ssss
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Said Mtanda akizungumza katika Barazala Madiwani wa Manispaa ya Ilemela, lililoketi leo kujibu hoja za ukaguzi wa CAG.
Madiwani wa Manispaa ya Ilemela,wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda (hayupo pichani),leo wakati wa kikao cha baraza hilo cha kujadili hoja za CAG.
Mstahiki Meya wa Ilemela,Renatus Mulunga,akizungumza na madiwani wa manispaa hiyo,leo baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya hoja za ukaguzi wa CAG za hesabu za mwaka wa fedha 2022/23,huku Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Ummy Wayayu (kulia),akipiga makofi.
Picha na Baltazar Mashaka