Na John Walter -Babati
Wananchi wa kata ya Kiru wilaya ya Babati mkoani Manyara wameiomba serikali kukarabati zahanati ya Kiru six inayotegemewa na vijiji sita vya kata hiyo na vijiji jirani, ili iweze kutoa huduma bora za afya.
Hayo yameibuliwa katika mkutano wa mbunge wa jimbo la Babati vijijni- Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa Daniel Sillo, uliofanyika kiru six kusikiliza kero za wananchi ambapo walimweleza juu ya uchakavu wa Zahanati ya kijiji ambayo kwa muda mrefu haijafanyiwa ukarabati.
Daktari katika zahanati hiyo Steven Gabriel amesema wanafanya kazi kwa hofu kutokana na uchakavu mkubwa wa jengo hilo ambalo pia lina nyufa maeneo mengi, halina dari (silin board) na kwamba wadudu wa kila aina wanaingia ndani ya zahanati na popo wamegeuza ndo makazi yao.
Dr. Gabriel anasema kituo hicho hakina umeme na badala yake wanatumia Sola ambayo uwezo wake ni mdogo hivyo hulazimika kutumia mwanga wa simu pindi wanapotoa huduma nyakati za usiku zikiwemo za kina mama kujifungua.
Amefafanua kuwa kutokana na umbali uliopo kutoka kwenye vijiji hadi kufika Zahanati, baadhi ya kina mama hulazimika kujifungulia majumbani akitolea mfano Kijiji cha Kokomay ambacho kipo zaidi ya kilomita 15.
“Hali hii inasababisha wakati mwingine kushindwa kufanya kazi zetu kwa ufanisi” alieleza Dr.Gabriel
Pamoja na hayo Zahanati hiyo haina huduma ya maji, hivyo wahudumu hulazimika kwenda kuchota mtoni -Mto Erri kwa ajili ya matumizi yao na wateja wanaofika kupata matibabu.
Mbunge wa Jimbo la Babati vijijini ambaye pia ni naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa Daniel Sillo ametembelea zahanati hiyo na kuahidi kujengwa kituo cha afya.
“Sasa nasema hivi watu wa Kiru na bahati nzuri diwani amenihakikishia kuwa eneo lipo la kutosha kujenga kituo cha afya, ninawaambia nawaletea kituo cha kisasa cha Afya Kata ya Kiru, Kiru ina wananchi wengi sana lazima mpate huduma safi ya afya” alisema Sillo
Diwani wa kata ya Kiru Benjamin Keremu amesema wametenga hekari 34 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya.