NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mji umempongeza kwa dhati Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Mhe. Silvestry Koka pamoja na mke wake Mama Selina Koka kwa juhudi na sapoti yao kubwa ya kuwakomboa wanawake kiuchumi kwa kuwawezesha mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi ambalo litakuwa ni mkombozi mkubwa katika kutimiza ndoto zao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu Mwenyekiti wa UWT Kibaha mji Elina Mgonja alisema kwamba Mbunge Koka amekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia kwa hali na mali wanawake pamoja na jamii kwa ujumla katika mambo mbali mbali ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Mgonja alisema kwamba kwa sasa UWT Wilaya ya Kibaha mjini imeweka mikakati kabambe ya kuaznisha miradi mbali mbali mabayo itakuwa ni moja ya mkombozi mkubwa katika kuwasaidia wanawake kuondokana na wimbi la umasikini na hatimaye kuweza kujikwamua kiuchumi.
“Kwa kweli sisi kama wanawake wa UWT Kibaha mji tunasema kwamba tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka pamoja na mke wake Mama selina Koka kwa moyo wao wa kujitoa kwa hali na mali katika kutusaidia sisi umoja wetu kwani kwa sasa tunamalizika kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo letu la kitega uchumi ambalo kwa sasa lipo tayari isipokuwa tunamalizia kukamilisha baaadhi ya vitu kadhaa,”alisema Mwenyekiti Mgonja.
Aliongeza kuwa Mbunge Koka amekuwa akitekeleza Ilani ya chama kwa vitendo na ndio maana ameweza kuwasaidia wanawake hao kuwa na mradi wa jengo lao kwa ajili ya kitega uchumi ambapo wameshirikiana bega kwa bega na mke wake ili kuhakikisha kwamba wanawawezesha wanawake hao kutimiza malengo yao waliyojiwekea.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa lengo kubwa la UWT ni kuweka misingi imara ambayo itaweza kumkomboa mwanamke na mtoto hivyo mradi huo wa kitega uchumi pindi utakapokamilika wataanzisha miradi mbali mbali ambayo itaweza kutoa hata fursa za ajili kwa wanawake wa UWT.
“Jambo kubwa amelifanya Mhe. Mbunge kwa ajili yetu sisi kina mama pamoja na mlezi wetu ambaye ni Mama Selina Koka kwa hivyo mimi nasema kwamba sio kwamba tunajipendkeza bali tunaongea ukweli na kwa sasa siasa ni uchumi na siku hizi tunasema mnyonge anyong’wi na haki yake anapewa maana jengo letu linapendeza,”alisema Mwenyekiti Mgonja.
Kwa upande wake Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Cesilia Ndalu hakusita kumpongeza mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mama Selina Koka ambaye pia ni mlezi wa UWT kwa kuwa bega kwa bega na jumuiya ya umoja wa wanawake katika kuwasapoti mambo mbali mbali ya kimaendeleo.
Katika hatua nyingine Katibu huyo alitumia fursa hiyo ya kuwakaribisha wajumbe wote katika mkutano wa baraza la UWT ambalo linatarajiwa kufanyika siku ya kesho Ijumaa katika ukumbi wa jengo la Halmashauri na kuwahimiza kuwahi mapema lengo ikiwa ni kushiriki kikamilifu katika baraza hilo.