MKURUGENZI wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi.Viola Masako, akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la TBS wakati wa Maonesho ya wiki ya Utumishi wa Umma 2024 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
AFISA Rasilimali Watu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi.Faidha Nyenzi,akitoa elimu kwa wananchi waliofika katika banda la TBS katika Maonesho ya wiki ya Utumishi wa Umma 2024 yanayoendelea Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limejikita katika kutoa elimu ya viwango na udhibiti ubora katika maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma 2024.
Hayo yamesemwa leo Juni 20, 2024 na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi.Viola Masako,wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la TBS katika Maonesho Hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Masako amesema TBS imeshiriki ili kutoa elimu juu ya masuala ya Viwango na udhibiti ubora kwa wadau na wananchi ikiwa ni pamoja na kuelimisha juu ya majukumu mbalimbali TBS inayotekeleza.
“Maonesho ya mwaka 2024 wananchi waliofika katika Banda la TBS waliweza kupatiwa Elimu na wengi wao walikuwa na dhamira ya kufahamu masuala ya udhibiti ubora ambao wataalamu wameweza kuwafahamisha lakini pia kwa namna gani wanaweza kuwafikia TBS.”amesema Masako
Amesema wananchi hao wamefahamishwa kuwa wanaweza kufikia ofisi kupitia ofisi za kanda kwani TBS ina Kanda 7 ikiwemo Kanda ya Mashariki iliyopo Dar Es Salaam, Kanda ya Kaskazini iliyopo Arusha, Kanda ya Kusini iliyopo Mtwara, Kanda ya Magharibi iliyopo Kigoma , Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyopo Mbeya, Kanda ya kati iliyopo Dodoma pamoja na kanda ya Ziwa inayopatikana Mwanza.
Masako ameongeza kuwa,“ Hii mikoa yote inahudumia mikoa yote ya Tanzania, hivyo ni rahisi kupata huduma zetu kiurahisi.”
Pia amesema TBS imekuwa ikitoa huduma zao kupitia mifumo mbalimbali ya kieletroniki katika kuhudumia pamoja na kutatua changamoto za wananchi.
Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yanaendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambayo yalianza Juni 16,2024 na yanatarajia kufungwa Juni 23,Mwaka huu.