Na WAF – ARUSHA
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezindua bodi mpya ya usimamizi wa kampuni tanzu ya ‘MSD MEDPHARM’ pamoja na kampuni tanzu ya ‘MSD Medipharm Manufacturing Compan Ltd’ itakayosimamia viwanda vya dawa na kusaidia upatikanaji wa huduma za Afya nchini.
Wakati wa uzinduzi huo ulifanyika leo Juni 20, 2024 Mkoani Arusha, Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za dawa na vifaa tiba ili kujihakikishia upatikanaji wa uhakika wa bidhaa hizo na kupunguza gharama za uagizaji kutoka nchi za nje.
“Uzalishaji wa ndani wa bidhaa za Afya ikiwemo dawa utaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani ili kuepuka kuchukua muda mwingi tunapoagia kutoka nchi za nje miezi 6 mpaka miezi 9, tulijifunza wakati wa UVIKO ila kwasasa tunazalisha dawa ndani ya nchi na zinapatikana kwa wakati.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy ameitaka Bohari ya Dawa (MSD) kuweka kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani wa dawa kwa kuhakikisha uendelevu wa viwanda hivyo ili kwenda sambamba na Serikali ambayo inaendelea kupambana kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuvilinda viwanda vya ndani vya dawa.
Wazir ummy pia ameipongeza Bodi ya MSD kwa kuja na kampuni tanzu kwani kwa kufanya hivyo wanazidi kuimarisha mpango wa Serikali katika kuifikia Sera ya kujitegemea katika kujizalishia bidhaa za dawa na kupunguza utegemezi wa dawa toka njee kwa asilimia 50 ifikapo 2030.
“Mmejiongeza vizuri kuunda bodi hii ili kulitekeleza vizuri jukumu tulilowapa la kuimarisha uzalishaji wa dawa muunde kampuni tanzu ili kuwiana na dira yetu ya Taifa ya Kujitegemea katika kuzalisha dawa muhimu na vifaa tiba kuelekea mwaka 2030.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, sasa hivi tunatumia asilimia 90 ya dawa na vifaa tiba kutoka njee ya nchi, ndani tuna asilimia 10 tu, kwa hiyo tunatakupunguza utegemezi wa dawa na bidhaa za Afya, bodi ambayo tunaizindua leo ni ishara kuelekea katika utekelezaji huo.” Amesema Waziri Ummy
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Bi. Rosemarry Silaa amesema tayari wameshapiga hatua kubwa ya kuhakikisha kampuni ina kuwa na kusimamamia kampuni nyingine za uzalishaji pamoja na kuisihi bodi hiyo mpya kuendelea na biashara zingine zilizokuwepo katika mipango.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa MSD na Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya usimamizi wa kampuni tanzu ya MSD MEDPHARM Manufacturing Bw. Mavere Tukai amesema ujio wa bodi hiyo ni matarajio ya kuisaidia MSD katika kutimiza majuku yake Manne ya msingi ya kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za Afya.